
HAMIDA RAMADHANI MZAWA ONLINE MEDIA DODOMA
NAIBU Waziri wa TAMISEMI, Dkt.Festo Dugange, amesema Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini zinakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo uhaba wa wataalamu, ukusanyaji mdogo wa mapato, na usimamizi usioridhisha wa miradi ya kimkakati na fedha za umma.
Dkt. Dugange ameyasema hayo Mwishoni mwa wiki hiliyo pita jijini Dodoma, alipomwakilisha Waziri Mohamed Mchengerwa kwenye Mahafali ya 16 ya Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) Hombolo.
Amebainisha kuwa chuo hicho kina nafasi muhimu katika kusaidia serikali kuzitatua changamoto hizo kupitia utafiti, mafunzo, na ushauri wa kitaalamu.

Akiipongeza LGTI Hombolo, Dkt. Dugange amesema chuo hicho kimekuwa kikijenga uwezo wa wataalamu wanaoweza kusaidia serikali kubuni miradi ya kimkakati yenye tija.
Amesisitiza kuwa halmashauri zinapaswa kuibua miradi inayoendana na mahitaji ya maeneo yao badala ya kuiga miradi kutoka halmashauri nyingine.
Ametoa mfano wa baadhi ya halmashauri kuanzisha miradi ya stendi za mabasi bila kuzingatia mahitaji halisi ya kiuchumi na kijamii ya maeneo yao.
Amesema hatua hiyo imekuwa changamoto kwani baadhi ya halmashauri hazihitaji miradi mikubwa ya aina hiyo.

Dkt. Dugange amehimiza chuo hicho kuendelea kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo wataalamu wa serikali za mitaa ili waweze kusimamia miradi kwa ubunifu na weledi.
Amelipongeza pia kwa mafanikio ya kubuni miradi yenye tija katika halmashauri mbalimbali nchini.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo amekitaka Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) Hombolo kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika kutatua changamoto zinazozikabili halmashauri badala ya kubaki kwenye makabati.
“Tafiti nyingi zimekuwa zikifanyika lakini hazitumiki ipasavyo katika kutatua matatizo hivyo ni wakati wa wanazuoni wa Hombolo kushirikiana na halmashauri kutatua changamoto zilizopo

Na kuongeza “Ni jukumu la wanazuoni wa Hombolo kupeleka maarifa haya kwenye halmashauri na kutatua changamoto kwa vitendo, badala ya kufungia tafiti kwenye makabati,” amesema Dkt. Dugange.
Amebainisha kuwa serikali inategemea wahitimu wa chuo hicho kuibua miradi bunifu inayolingana na mahitaji ya Halmashauri mbalimbali ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.