
KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma Jawadu Mohamed amesema kuwa chama hicho kimeendelea kupambana na maadui watatu wakuu wa maendeleo, ambao ni ujinga, maradhi, na umasikini, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Uhuru.
Akizungumza leo jijini hapa na waandishi wa habari, Katibu huyo alieleza kuwa tangu kupata uhuru, CCM imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii kama elimu bora, afya, na fursa za kiuchumi zinazoinua hali za maisha ya kila Mtanzania.
Amesema kuwa mapambano haya yamekuwa yakitekelezwa kupitia sera na mipango madhubuti ya maendeleo inayolenga kuinua uchumi wa taifa na maisha ya watu.
Ameongeza kuwa serikali ya CCM imefanikiwa kupunguza ujinga kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule mpya, utoaji wa elimu bure, na upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kufundishia.
Vilevile, ameeleza juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya, hospitali, na kuimarisha upatikanaji wa dawa na huduma bora kwa wananchi.
Katibu huyo pia alisisitiza umuhimu wa kushirikiana kati ya wananchi na serikali katika kutekeleza mipango ya maendeleo.
Amesema kuwa ushindi wa mapambano haya hauwezi kupatikana bila ushirikiano wa kila mmoja, akiwataka wananchi kuendelea kushikamana na kuunga mkono juhudi za serikali.
“Siku ya Uhuru inatufundisha thamani ya kujitolea, mshikamano, na dhamira ya kweli ya kupigania maendeleo ya taifa letu. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha tunailinda na kuitumia vyema uhuru huu kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema Katibu huyo.
Katika kuhitimisha, amewataka Watanzania kuendelea kuwa wamoja na kujiandaa kushiriki kikamilifu katika mipango mbalimbali ya maendeleo inayosimamiwa na CCM, akisisitiza kwamba mafanikio ya taifa yanahitaji mshikamano wa wote.
Katika hatua nyingine, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Jawadu ameeleza masikitiko yake juu ya tabia za baadhi ya vijana waliotoa matamshi ya kuwaombea wabunge waliohusika katika ajali ya Dodoma Mbande kufariki dunia.
Amesema kuwa matamshi kama hayo yanapotosha maadili ya kijamii na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa. Alisema kuwa ni muhimu kwa vijana na Watanzania kwa ujumla kuonyesha utu na huruma kwa wenzao, hasa wanapokumbwa na majanga kama ajali.
“Ajali ni tukio la kusikitisha ambalo linaweza kumkuta yeyote. Kwa kweli, kama taifa, hatuwezi kuruhusu chuki au maneno ya dhihaka katika mazingira kama haya tunapaswa kuwa taifa lenye mshikamano na upendo kwa kila mmoja, bila kujali tofauti za kisiasa au kijamii,” amesema.
Katibu huyo ametoa wito kwa viongozi wa dini, wazazi, na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawaelekeza vijana katika misingi ya heshima, maadili, na mshikamano wa kitaifa
Amesema kuwa CCM itaendelea kulaani vitendo vya aina hiyo na kuhimiza maadili mema miongoni mwa vijana.
Aidha, amewatakia wabunge waliopata ajali hiyo uponyaji wa haraka na kuwataka Watanzania wote kuwaombea kwa Mungu wapone na kurejea katika majukumu yao ya kitaifa.
Ameongeza kuwa mshikamano katika nyakati za changamoto ni kiashiria cha umoja wa taifa, na kila mmoja anapaswa kushiriki katika kuimarisha mshikamano huo.
Hata hivyo Jawadu amepongeza falsafa ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kuhusu uongozi bora na kugatua madaraka kwa faida ya wananchi.
Amesema kuwa Mwalimu Nyerere alisisitiza umuhimu wa viongozi kujituma katika kuwahudumia wananchi kwa haki na usawa, bila kushikilia madaraka kwa muda mrefu au kuyatumia kwa manufaa binafsi.
“Baba wa Taifa aliweka msingi wa kwamba uongozi ni dhamana, siyo fursa ya kujinufaisha. Alionyesha kwa vitendo alipoamua kuachia madaraka kwa hiari mwaka 1985, jambo ambalo ni somo kubwa kwa viongozi wa sasa,” amesema.
Katibu huyo ametoa wito kwa viongozi wa sasa katika ngazi zote za serikali na chama kuiga mfano wa Mwalimu kwa kuzingatia maadili ya uongozi bora, kujituma, na kuhakikisha wanawahudumia wananchi ipasavyo.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa viongozi kugatua madaraka ili kuwezesha maendeleo kwa wananchi wote, hasa vijijini ambako bado kuna changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii.
“Mwalimu Nyerere aliamini kwamba kugatua madaraka kunawapa wananchi nguvu ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi yanayohusu maendeleo yao. Hii ndiyo njia sahihi ya kujenga taifa lenye mshikamano, haki, na usawa,” aliongeza.
Aidha, alihimiza viongozi wa sasa kuendelea kuheshimu na kuendeleza maono ya Mwalimu kwa kufanya kazi kwa bidii, uwazi, na uadilifu. “Tukifuata nyayo za Mwalimu Nyerere, tutaweza kutatua changamoto za sasa na kulinda heshima ya taifa letu,”
Mwisho