

📌Mawaziri wa Viwanda na Biashara wa nchi hizi mbili waahidi kufungua fursa zaidi za kibiashara na uwekezaji;
📌Waziri Kapinga anadi fursa za kibiashara kwa Tanzania na mkakati wa kuongeza mnyororo wa thamani kwa bidhaa za Tanzania;
📌Ujumbe wa Congo watembelea mamlaka ya bandari Tanzania ambayo ndio mhimili wa uchumi kwa nchi yao.
Na Neema Chalila Mbuja
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Judith Kapinga(Mb), na Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe Julien Paluku Kahongya wamesaini
Makubaliano ya uwezeshaji na ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili kwa lengo la kukuza uchumi na kufungua fursa zaidi za kibiashara.
Makubaliano hayo yamesaniwa jijini Dar es salaam na Mawaziri hao kufuatia ziara ya hivi karibuni aliyoifanya Rais wa nchi hiyo kwa ajili ya fursa za kibiashara ambapo nchi ya Congo inategemea sana bandari ya Dar es salaam kwa ajili ya usafirishaji wa bidhaa kwenda nchini Kongo.
Aidha Mhe Kapinga ameainisha maeneo ya ushikiano yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na usafirishaji, mauzo ya nje ya bidhaa, uwezeshaji wa kibiashara, miundombinu na biashara zinazovuka mipaka.

Ujumbe huo wa Waziri Biashara wa Kongo ulitembelea Mamlaka ya Bandari Tanzani kujionea namna bandari inavyofanya kazi kama kiungo muhimu katika biashara baina ya Tanzania na Kongo, huku nchi hizo zikikubaliana kuanzisha kamati ya pamoja ya kibiashara kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara baina ya nchi hizo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam akiwa ameambatana na Waziri wa Biashara wa Kongo, Mhe. Julien Paluku Kahongya, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Bw. Sempeho Manongi, amesema Kongo ni nchi muhimu kwa Tanzania katika mahusiano ya biashara.

Amesema bidhaa zinazozalishwa Kongo, ikiwemo madini, zinaweza kupita katika Bandari ya Dar es Salaam na kutumia miundombinu ya Tanzania, huku bidhaa zinazozalishwa Tanzania zikienda katika soko la Kongo.
Ameeleza kuwa Tanzania na Kongo zimeingia makubaliano ya kuanzisha kamati ya pamoja ya kibiashara itakayohimiza na kuboresha mazingira ya biashara baina ya nchi hizo mbili.
Manongi amesema Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya biashara ili kuongeza biashara na nchi zinazozunguka, huku akiwahimiza wadau wa sekta binafsi kuchangamkia fursa zilizopo baina ya Tanzania na Kongo.









