Home Kitaifa KCMC YAPATA TIBA MIONZI: SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 5.5 KUSOGEZA HUDUMA ZA SARATANI...

KCMC YAPATA TIBA MIONZI: SERIKALI YAWEKEZA BILIONI 5.5 KUSOGEZA HUDUMA ZA SARATANI KARIBU NA WANANCHI

Na John Mapepele, WAF – Kilimanjaro

Tanzania imeandika ukurasa mpya katika mapambano dhidi ya saratani baada ya Serikali kuzindua rasmi Jengo la Tiba Mionzi katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kilimanjaro Christian Medical Centre (KCMC), hatua inayotarajiwa kuwanufaisha maelfu ya wagonjwa wa Kanda ya Kaskazini na nchi jirani.

Uzinduzi huo uliofanyika leo Juni 24, 2026, umeelezwa kuwa moja ya mafanikio makubwa ya uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya afya, hususan katika kuimarisha huduma za kibingwa na bobezi nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, kabla ya kumkaribisha mhe Rais Samia Suluhu hassan, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa (Mb.), alisema jengo hilo siyo tu uwekezaji wa miundombinu, bali ni ishara ya matumaini mapya kwa wagonjwa wa saratani na familia zao.

“Leo tunashuhudia mageuzi makubwa katika mfumo wa afya wa Tanzania. Hili si jengo la kawaida; ni hatua ya kuokoa maisha, kupunguza maumivu na gharama kwa wananchi wetu,” alisema Waziri Mchengerwa.

Alibainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeweka kipaumbele katika kusogeza huduma za matibabu karibu na wananchi ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 5.5 katika ujenzi wa jengo hilo pamoja na ununuzi wa sehemu ya vifaa vya tiba mionzi.

Alisema huduma za tiba mionzi katika KCMC tayari zimeanza kutolewa tangu Februari mwaka huu, huku kituo hicho kikiwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 1,100 kwa mwaka katika awamu ya sasa.

Aidha, baada ya kukamilika kwa awamu zote za mradi, kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia hadi wagonjwa 3,900 kwa mwaka, hatua itakayopunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na kupunguza gharama za matibabu kwa familia nyingi.

“Huduma ya karibu kwa mgonjwa wa saratani si suala la miundombinu pekee. Ni suala la matumaini, ⁸ni tofauti kati ya kuchelewa na kuwahi kupata matibabu, na wakati mwingine ni tofauti kati ya maisha na kifo,” alisisitiza.kwa

Katika hatua nyingine Waziri Mchengerwa alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya, vifaa tiba vya kisasa na mafunzo ya wataalamu ili kuboresha huduma za uchunguzi na matibabu ya saratani nchini.

Alieleza kuwa Wizara ya Afya itaendelea kushirikiana na KCMC pamoja na wadau mbalimbali kuhakikisha vifaa vya awamu zinazofuata vinapatikana kwa wakati na huduma zinaendelea kutolewa kwa viwango vya kitaifa na kimataifa.

Katika hotuba yake, Waziri huyo alitambua mchango mkubwa wa taasisi za dini katika utoaji wa huduma za afya nchini, akizitaja KCMC na Hospitali ya Bugando kuwa mifano hai ya ushirikiano wenye mafanikio kati ya Serikali na taasisi hizo.

Alisema ushirikiano huo umechangia kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, kupunguza rufaa zisizo za lazima na kuimarisha mfumo wa afya wa taifa.

“KCMC na Bugando zinaonyesha wazi kuwa Serikali inaposhirikiana na taasisi za dini, wananchi ndiyo wanakuwa washindi wakubwa,” alisema.

Waziri pia alitoa shukrani kwa wadau wa maendeleo walioshiriki kufanikisha mradi huo, hususan Foundation for Cancer Care in Tanzania (FCCT) na Shirika la USAID, kwa mchango wao katika ujenzi wa jengo hilo na upatikanaji wa vifaa tiba.

Alisema ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na wadau wa maendeleo umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuboresha huduma za afya nchini.

Akihitimisha hotuba yake, Waziri Mchengerwa alimpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya afya kupitia uboreshaji wa miundombinu, mafunzo ya wataalamu na ustawi wa watumishi wa afya.

Alisema jengo la tiba mionzi la KCMC litabaki kuwa alama ya maono ya Rais Samia ya kujenga mfumo wa afya unaotoa huduma bora, za kisasa na zinazowafikia wananchi kwa urahisi.

Uzinduzi wa kituo hicho unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu ya saratani nchini, kupunguza vifo vinavyotokana na kuchelewa kupata matibabu na kutoa matumaini mapya kwa maelfu ya Watanzania wanaopambana na ugonjwa huo.

Wakati huo huo, Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha kusikitishwa na ongezeko la magonjwa ya saratani na moyo kwa wananchi hususan katika umri mdogo ukilinganishwa na awali.

Ameelekeza taasisi zinazohusika na tafiti za masuala ya afya kufanya tafiti ili kujua sababu zinazofanya kuwe na ongezeko la magonjwa hayo katika umri mdogo na kutoa elimu ya uelewa ili wananchi wajikinge na ugonjwa huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!