Home Kitaifa BARAZA LA USHINDANI LAJA NA MFUMO WA KIDIJITALI KURAHISISHA RUFAA ZA WANANCHI

BARAZA LA USHINDANI LAJA NA MFUMO WA KIDIJITALI KURAHISISHA RUFAA ZA WANANCHI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Baraza la Ushindani (FCT limeendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa kutumia teknolojia za kidijitali, likiwataka wananchi na wadau kutumia mfumo wa kielektroniki kuwasilisha mashauri na rufaa zao kwa urahisi na kwa wakati.

Msajili wa Baraza la Ushindani, Mbegu Kaskasi, amesema Baraza hilo lililo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara lina jukumu la kusikiliza na kutatua migogoro ya ushindani wa biashara na udhibiti wa soko inayotokana na maamuzi ya Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na mamlaka za udhibiti zikiwemo TCRA, EWURA, LATRA, TURA na TCAA.

Kaskasi amesema Baraza hilo linaundwa na Jaji wa Mahakama Kuu pamoja na wajumbe sita, huku likitumia fursa mbalimbali kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu yake, namna ya kupata huduma na utaratibu wa kuwasilisha mashauri, ikiwemo kupitia mfumo wa kielektroniki wa usikilizaji wa mashauri.

Amesema mfumo huo umewekwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, ambapo kwa sasa wanaweza kuwasilisha mashauri na rufaa zao kwa njia ya kielektroniki bila kulazimika kufika ofisini, hatua inayokwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali nchini.

Kwa upande wake,Afisa Sheria wa baraza hilo ,Hafsa Said, amesema mchakato wa rufaa huanza kwa mhusika kuwasilisha notisi ya rufaa pamoja na kuwapatia nakala wahusika wanaopaswa kujibu rufaa hiyo. Baada ya hapo, mhusika anatakiwa kuwasilisha sababu za rufaa pamoja na kumbukumbu zinazohusiana na shauri hilo.

Amesema baada ya mjibu rufaa kuwasilisha majibu yake, shauri hukamilika kwa ajili ya kusikilizwa, huku Baraza likiwa na utaratibu wa kuhakikisha rufaa inayowasilishwa kikamilifu inasikilizwa na kutolewa uamuzi ndani ya kipindi kisichozidi miezi sita.

Naye Afisa TEHAMA wa Baraza hilo Bw.Athumani Kanyegezi  amewataka wananchi na wadau kutumia mfumo wa kielektroniki unaopatikana kupitia tams.fct.or.tz au tovuti ya Baraza fct.or.tz, akieleza kuwa mfumo huo ni rafiki kwa mtumiaji na umeundwa kuendana na mahitaji ya sasa ya utoaji huduma kwa njia ya kidijitali.

Amesema matumizi ya teknolojia hiyo ni sehemu ya juhudi za Baraza kwenda sambamba na mabadiliko ya kidijitali na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, huku akiwataka wananchi kutumia fursa hiyo kupata huduma kwa urahisi.

Aidha, imeelezwa kuwa uwepo wa Baraza la Ushindani unawapa wananchi fursa ya kukata rufaa pale wanapokuwa hawajaridhishwa na maamuzi ya mamlaka zinazodhibiti sekta mbalimbali. Kwa mfano, mwananchi mwenye malalamiko dhidi ya kampuni ya simu anaweza kwanza kuyawasilisha katika mamlaka husika na, endapo hataridhishwa na uamuzi, anaweza kutumia fursa ya kukata rufaa katika Baraza la Ushindani.

Naye Mdau Vendeline Shekifu,ameeleza kufurahishwa na uwepo wa taasisi hiyo umewapa fursa ya kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na taasisi za Serikali, ikiwemo Baraza la Ushindani.

Awali Diwani wa Kata ya Tamkaleli Clinton Manzi  amesema maadhimisho hayo yamekuwa na manufaa kwa wakazi wa Dodoma kutokana na muda walioupata kujifunza huduma na fursa mbalimbali, huku akimshukuru Rais kwa kuwezesha maadhimisho hayo kufanyika jijini Dodoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!