Home Kitaifa DCEA YAKAMATA LITA 66,048 ZA KEMIKALI BASHIRIFU, WATUHUMIWA WAWILI WATIWA MBARONI

DCEA YAKAMATA LITA 66,048 ZA KEMIKALI BASHIRIFU, WATUHUMIWA WAWILI WATIWA MBARONI

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekamata jumla ya lita 66,048 za kemikali bashirifu zilizoingizwa nchini kinyume cha sheria.

Hayo yamesemwa leo Mei 13, 2026 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Amesema ukamataji huo ni matokeo ya operesheni maalum iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwezi Aprili 2026.

Kemikali zilizokamatwa ni Cyclohexanone yenye ujazo wa lita 16,048 pamoja na Extra Neutral Alcohol (ENA) yenye ujazo wa lita 50,000,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Pia amesema kupitia operesheni hiyo, magari mawili yaliyohusika katika usafirishaji yanashikiliwa, huku watuhumiwa wawili wakikamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Hata hivyo, amesema uchunguzi umebaini kuwa kemikali aina ya Cyclohexanone ziliingizwa nchini na kampuni ya Kinglion Investment Company LTD bila kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kukosa vibali kutoka mamlaka husika.

Aidha, amesema kemikali aina ya Extra Neutral Alcohol (ENA) zilikuwa zikisafirishwa kwa kutumia magari ya mafuta aina ya petrol yaliyokuwa yamebandikwa vibali vya kughushi.

Amesema hali hiyo ni sehemu ya mtandao wa kihalifu unaolenga kuzichepusha kemikali hizo kwa matumizi haramu.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema kemikali aina ya Cyclohexanone hutumika kuzalisha dawa za kulevya aina ya PCP (Phencyclidine), na kwamba kiasi kilichokamatwa kingeweza kuzalisha takribani tani 11.4 za dawa hizo haramu nchini.

“Kutokana na udhibiti wa dawa za kulevya kuimarika duniani, mitandao ya kihalifu imekuwa ikitumia kemikali bashirifu kuzalisha dawa za kulevya katika maabara bubu,” amesema.

Katika hatua nyingine, mamlaka hiyo imesema sambamba na operesheni hiyo, ilifanya misako katika mikoa mbalimbali ikiwemo Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Morogoro na Dodoma.

Pia, ekari 38.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa huku watuhumiwa 84 wakikamatwa kuhusiana na matukio hayo.

Mamlaka hiyo imeonya kuwa itaendelea kuchukua hatua kali dhidi ya watu wote watakaobainika kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya pamoja na uchepushaji wa kemikali bashirifu.

Aidha, imewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!