Home Kitaifa WIZARA YA AFYA ISHIRIKISHE WADAU KUCHANGIA HUDUMA ZA TIBA – WAZIRI MKUU

WIZARA YA AFYA ISHIRIKISHE WADAU KUCHANGIA HUDUMA ZA TIBA – WAZIRI MKUU

Akabidhi sh. milioni 600 kusaidia wanawake wenye tatizo la Fistula
Aipongeza NMB kufikisha lengo la sh. bilioni 1 ndani ya miaka miwili

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Afya iendelee kuhamasisha taasisi, na wadau kuchangia maeneo muhimu kama ya afya hasa yanayogusa jamii ikiwemo fistula, na saratani ambayo yanasumbua jamii.

Suala la kuchangia maendeleo na utatuzi wa changamoto za jamii ni la Watanzania wote. Kwa umoja wetu tukishirikiana, tutaifanya Tanzania yetu kuwa salama zaidi. Hivyo, nitoe rai kwa makampuni mengine yanayofanya biashara hapa nchini kushirikiana na Serikali ili kwa pamoja tutatue changamoto hizo,” amesema.

Akizungumza na mamia ya washiriki wa mbio za hisani za NMB leo (Jumamosi, Oktoba Mosi, 2022) kwenye viwanja vya Leaders’ Club jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema Serikali pamoja na jitihada zake za kutoa huduma, bado inahitaji kuungwa mkono na Watanzania na yeyote ambaye ameguswa na jambo hilo ili kunusuru maisha ya mama zetu.

Taarifa za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa akinamama wengi, wanasumbuliwa na tatizo la fistula lakini wengi wao wamepoteza matumaini kwa sababu hawawezi kumudu gharama za matibabu. Hivyo, wanapotokea watu wa kuwasaidia, hatutasita kushirikiana nao ili kuhakikisha mama zetu, dada zetu na hata watoto wetu wanapata msaada,” amesema.

Ameipongeza benki ya NMB kwa kufanikiwa kuchangisha sh. bilioni moja ndani ya miaka miwili badala ya miaka minne kama iliyopangwa awali. “Utaratibu kama huu wa benki ya NMB kusaidia jamii ambao umeonesha mafanikio makubwa ya kuchangia shilingi bilioni moja kwa miaka miwili tu, ni wa kuigwa na taasisi nyingine. Mwaka jana tulipata shilingi milioni 400 badala ya sh. milioni 250 zilizokusudiwa. Mwaka huu tumepata sh. milioni 600 badala ya milioni 250.”

Amezipongeza kampuni za bima za Sanlam kwa kuchangia sh. milioni 150 na kampuni ya bima ya UAP kwa kuchangia sh. milioni 100. Mbio hizo zilianzia kwenye viwanja vya Leaders’ jijini Dar na kuzunguka viunga vya jiji la Dar na kuishia kwenye viwanja hivyo.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Michezo Nchini (BMT) lisimamie mashirikisho ya michezo yote kuandaa mipango itakayojumuisha watu wengi kushiriki michezo kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Pia amekiagiza Chama cha Riadha Tanzania (RT) kiendelee kuhakikisha mbio nyingi zinazofanyika nchini zinaratibiwa vizuri na kuhamasisha jamii kushiriki. Pia amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa ziendelee kusajili vikundi mbalimbali vya riadha, jogging na aina nyingine ya mazoezi.

Manispaa za Temeke, Kinondoni, Ilala na nyinginezo, ziwatambue rasmi wanaoshiriki kwenye hivi vikundi na kuwasaidia kutambuliwa kwa shughuli zao kwa sababu vinasaidia kukuza hamasa ya michezo katika jamii,” amesisitiza.

Pia ameyataka mashirika, makampuni na majeshi nchini yarudishe utaratibu wa kuunda vikundi vya kuibua vipaji ili kurudisha hadhi ya nchi katika mashindano ya kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!