Home Kitaifa MANISPAA YA MOROGORO YATANGAZA KAMPENI YA USAFI.

MANISPAA YA MOROGORO YATANGAZA KAMPENI YA USAFI.

Na Saidi Ibada, Morogoro.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga ametangaza kampeni ya usafi wa mazingira katika kata zote za Manispaa ya Mkoa huo lengo ni kuhakikisha mji wa Morogoro unaingia kwenye orodha ya miji misafi hapa nchini kwa kuthibiti utapaji hovyo wa takataka.

Hayo ameyazungumza leo wakati wa tukio la kufanya usafi wa kuokota taka za plastiki pembezoni mwa barabara katika kata ya Mazimbu kuelekea Chuo cha Solomon Mahlangu (SUA).

Tukio hilo limeratibiwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Afri_Nature Organization (ANO) inayojishulisha na utunzaji wa mazingira mkoani Morogoro.
Mstahiki Meya amesema kampeni hiyo inalenga kushindanisha kata zote za Manispaa hiyo na mshindi atapewa zawadi, shabaha ikiwa ni kuinua morali ya usafi katika maeneo husika.

“Tumeshakubaliana, tunaenda kushindanisha kata kwa Kata kwa kuangalia usafi wa barabara zetu na maeneo yote na tutatoa zawadi kwa watakaofanya vizuri. Kila mtu kwenye eneo lake afanye usafi asisubirie wengine waje wamfanyie usafi”, amesema Kihanga.

Aidha, amewataka wananchi kuwa mabalozi wa mazingira kwa kufanya usafi katika maeneo yao na kando ya barabara, pia amewataka kuwaripoti wote wanaotupa taka hovyo na Ofisi yake itawashughulikia kwa mujibu wa sheria ya mazingira.

“Kila Jumamosi tutafanya usafi na kutoa elimu kwa Wananchi, baada ya hapo tutaanza kutoa adhabu, na bahati nzuri tuna sheria ndogo ya Manispaa ambayo mtu akichafua mazingira anatakiwa alipe elfu hamsini. Ninahimiza sana wananchi kulizingatia hili”, amesema Kihanga.

Kwa upande wake Balozi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Chage Alex Chage amezitaka kampuni zinazotengeneza vinywaji na kufungashia kwenye chupa za plastic kuanzisha kampuni mama za kufanya usafi au kutoa fidia kwa makampuni binafsi ya usafi ili kuthibiti kuzagaa kwa chupa hali inayopelekea uharibifu wa mazingira.

“Changamoto tulizoziona ni namna gani ya kuthibiti chupa za plastiki za makampuni ya energy na makampuni mengineyo, hili jambo limekuwa kero kwa mazingira, chupa za plastiki ni nyingi sana, hivyo kwa tutashirikiana na Ofisi ya Manispaa na Waziri kuangalia namna gani hili jambo litashughulikiwa. Kama kuna uwezekano makampuni haya yaanzishe makampuni mama ya usafi au kutoa fidia kwa watu watakao okota chupa zao, mana wao ndio wanapata faida. Hivyo lazima tujue wao wanachangia nini kwenye suala zima la uharibifu wa mazingira”, amesema Chage.

Naye Katibu wa taasisi ya ANO, Esther Mnyasa amesema wao kama wadau wa mazingira wataendelea kushirikiana na viongozi wa Mkoa katika kampeni ya usafi kila mwisho wa mwezi ili kuhakikisha wananchi wanapata elimu ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!