
Mwenge wa uhuru 2025 umepokelewa leo Aprili 11, 2025 Mkoani Morogoro kutoka Mkoa wa Pwani na unatarajia kupitia miradi 70 ya maendeleo yenye thamani ya Tsh. Bil. 18.5 ambayo inapatikana Halmashauri zote 9 za Mkoa huo.
Hayo yamebainishwa Aprili 11, 2025 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima wakati wa makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kutoka Mkoa wa Pwani katika kijiji cha Mgude Wilayani Morogoro ukiwa ni Mkoa wa pili kupokea mwenge huo tangu ulipozinduliwa na Mhe. Dkt. Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mkoani Pwani Aprili 2 mwaka huu.

Malima amesema miradi hiyo ya maendeleo inayowagusa wananchi ikiwemo miradi ya afya, mindombinu, elimu, maji na miradi mingine inatarajia kuleta maendeleo na kukuza uchumi wa wananchi huku akiahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa wakimbiza Mwenge wa Kitaifa ili waweze kukamilisha majukumu yao ya kukimbiza Mwenge huo.
Naye mkimbiza mwenge kitaifa Ismail Ali Ussi amesema matarijio hao ni kuifikia miradi yote katika Mkoa wa Morogoro na kuizindua ili wananchi waweze kupata huduma mbalimbali za kijamii.
Mwenge wa uhuru unatarajiwa kukimbizwa Mikoa 31 hapa nchini, Halmashauri 195 ukiwa na kaulimbiu inayosema “Jitokeze kushiriki uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu”.
Mwisho.