
Maandalizi ya kuelekea mashindano ya AFCON 2027 yanaendelea vizuri, huku Jiji la Arusha likijipanga kupokea wageni kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika watakaowasili nchini kwa ajili ya michuano hiyo.
Akizungumza Juni 20, 2026, katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Afisa Habari wa Jiji la Arusha, Masanja Kalegi, amesema Arusha tayari kuna hoteli za kutosha za kuhudumia wageni, huku baadhi zikiendelea kufanyiwa maboresho na nyingine mpya zikijengwa ili kuongeza uwezo wa malazi.

Amesema pia ujenzi wa miundombinu unaendelea, ikiwemo barabara zinazozunguka uwanja pamoja na kuunganisha maeneo mbalimbali ya mji ili kurahisisha usafiri na huduma wakati wa mashindano hayo.
Kalegi amesema AFCON 2027 italeta fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi wa Arusha, ambapo wafanyabiashara wadogo na wakubwa watapata nafasi ya kunufaika kutokana na ongezeko la wageni na mahitaji ya bidhaa na huduma.
Ameongeza kuwa wananchi wa Arusha watapewa kipaumbele katika shughuli za biashara, huku maeneo maalumu ya biashara ndani na nje ya uwanja yakitengwa kwa ajili ya wauzaji wa bidhaa mbalimbali, ikiwemo matunda, nyanya na mboga mboga.
Amesema ujio wa AFCON 2027 ni fursa muhimu kwa Arusha kuimarisha uchumi wa wananchi wake na kuonesha uwezo wa jiji hilo katika kuhudumia matukio makubwa ya kimataifa.









