Home Kitaifa DKT. BITEKO AFAFANUA UTEKELEZAJI WA VIPAUMBELE VYA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA...

DKT. BITEKO AFAFANUA UTEKELEZAJI WA VIPAUMBELE VYA BAJETI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23

Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema sekta ya Madini, Mwaka wa Fedha 2021/22 ulikuwa ni mwaka wa kazi na matokeo,kwa kuweza kukusanya Maduhuli ya Serikali ya shilingi bilioni 622.5 sawa na asilimia 96.

Akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Geita Leo Julai 12,2022 Dkt. Biteko amesema mwaka 2021 sekta ya Madini iliendelea kuifungua nchi yetu kiuchumi kwa kuchangia asilimia 45.9 ya thamani ya bidhaa zote zilizouzwa nje ya nchi na kuliingizia Taifa dola za Marekani milioni 3,103.20, huku kasi ya ukuaji wa sekta mwaka 2021 ilikua na kufikia asilimia 9.6 ikilinganishwa na asilimia 6.7 mwaka 2020 na kuwa ya tatu miongoni mwa sekta nyingine kutokana na ongezeko la uwekezaji.

Dkt.Biteko amesema Mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa uliendelea kuimarika ambapo katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2021, uliongezeka hadi kufikia wastani wa asilimia 7.3 kutoka wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. Pia, katika robo ya mwaka ya Julai hadi Septemba 2021 mchango wa sekta uliongezeka hadi kufikia asilimia 7.9 ikilinganishwa na mchango wa asilimia 7.3 kwa kipindi kama hicho mwaka 2020.

Mwaka 2021/22 kwa Sekta ya Madini ulikuwa wa matokeo kwa sababu tulifanikiwa kutoa leseni za uchimbaji mkubwa kwa madini ya nikeli na dhahabu, sambamba na kusainiwa kwa mikataba ya madini ikiwemo ya kinywe (graphite), madini mazito ya mchanga wa baharini ambayo itapelekea kuanzishwa kwa migodi mikubwa na ya kati jambo ambalo litazidi kuongeza thamani ya madini yetu, kukuza ajira, kukuza uchumi wetu na kuongeza mchango wa sekta kwenye Pato la Taifa na kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 kama ilivyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo”alisema Dkt.Biteko.

Aidha amesema ni mwaka ambao kama Wizara na Sekta walipata bahati ya kutembelewa na wageni kutoka nchi za Burundi, Zimbabwe, Sudani ya Kusini, Zambia na nyingine ambazo zilikuja kujifunza Tanzania namna ilivyofanikiwa kuisimamia sekta ya madini na ikatoa manufaa makubwa ya kiuchumi kwa nchi na hii ni ishara tosha kwamba, Sekta ya Madini imeleta mapinduzi makubwa Tanzania na ya kuigwa na mataifa mengine.

Mhe.Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ambaye anataka kuona thamani halisi ya madini yetu ikichangia kwa tija kubwa kwenye maendeleo ya watu wetu na taifa letu. Na pia kupitia filamu yake ya The Royal Tour” alieleza Dkt.Biteko.

Aidha amesema mafanikio haya yametokana na kutekelezwa kikamilifu kwa vipaumbele walivyojipangia mwaka 2021/22 vya kuhakikisha madini yetu yanaleta thamani halisi ya maendeleo.

Akizungumzia mchango wa Bunge kwa Wizara ya Madini Mhe.Biteko amesema katika Mwaka wa Fedha 2022/23, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha bajeti ya jumla ya shilingi 83,445,260,000.00 kwa ajili ya Wizara na Taasisi zake ili kuiwezesha Wizara kutekeleza majukumu yake,na kati ya fedha hizo, shilingi 22,000,000,000.00 ni fedha za maendeleo. Shilingi 61,445,260,000 ni fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida, shilingi 20,209,600,000.0 ni kwa ajili ya mishahara na shilingi 40,835,660,000.00 ni matumizi mengineyo.ambapo bajeti hii ni sawa na ongezeko la asilimia 19.95 ya bajeti iliyopitishwa Mwaka wa Fedha 2021/22.

Pia amesema utekelezaji wa bajeti hii ya Mwaka wa Fedha 2022/23, utazingatia utekelezaji wa vipaumbele vya wizara kama walivyopanga ambavyo vinalenga kuhakikisha rasilimali madini zinazidi kulinufaisha taifa letu kiuchumi na kimaendeleo kwa kuzingatia miongozo mbalimbali ya kitaifa ikiwemo Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) 2020-2025, Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22-2025/26, Sera ya Madini ya Taifa 2009, Mpango Mkakati wa Wizara wa Mwaka 2019/20 2023/24 na Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025.

Vipaumbele ambavyo wizara imepanga kutekeleza Mwaka wa Fedha 2022/23 ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa; kuwaendeleza wachimbaji wadogo na kuwawezesha wananchi kushiriki uchumi wa madini; kuhamasisha biashara na uwekezaji katika Sekta ya Madini; kusimamia mfumo wa ukaguzi wa shughuli za migodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!