Home Kitaifa ZOEZI LA SENSA SI LA KISIASA BALI KISHERIA- RC MKIRIKITI

ZOEZI LA SENSA SI LA KISIASA BALI KISHERIA- RC MKIRIKITI

Wajumbe wa Kamati ya Sensa mkoa wa Rukwa wakiwa kwenye kikao leo mjini Sumbawanga cha kupanga mkakati wa kuhamasisha wananchi kushiriki kwenye sensa ya mwaka huu
Mratibu wa Sensa Mkoa wa Rukwa Adam Ramadhan (aliyesimama) amesema kuwa maandalizi ya sensa yamefikia asilimia 87 kwenye halmashauri zote za Rukwa hadi sasa. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliyeongoza kikao hicho leo mjini Sumbawanga.

Na. OMM Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti amewataka wajumbe wa kamati ya sensa ya mkoa kuhakikisha wananchi wengi wakiwemo wenye ulemavu wanapata elimu ya sensa na kuwa tayari kuhesabiwa ifikapo Agosti 23 mwaka huu.

Ametoa kauli hiyo leo (07.07.2022) mjini Sumbawanga wakati wa kikao cha kwanza cha kamati ya sensa ya mkoa kilicholenga kutoa elimu na hamasa kwa wajumbe kujua majukumu yao ikiwemo hatua iliyofikiwa kwenye maandalizi ngazi ya mkoa.

“Katika jambo hili la sensa hakuna kuchelewa, kazi ya hamasa na elimu kwa wananchi itolewe kwa usahihi na kwa wakati ikiwemo kwa watu wenye ulemavu kote ndani ya halmashauri za mkoa wa Rukwa “alisema Mkirikiti.

Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe wa kamati ya amani na viongozi wa mila , Mkirikiti aliongeza kusema kila mmoja mahala alipo awe na utaratibu wa kutamka neno sensa hatua itakayoongeza hamasa ya wananchi kutambua umuhimu wa kujiandaa kushiriki kwenye zoezi la sensa.

Mkirikiti alibainisha kuwa zoezi la sensa si la kisiasa bali ni la kisheria kwani taifa linalenga kupata takwimu na taarifa sahihi za watu wake kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo.

“Zoezi hili la sensa si la kisiasa bali la kisheria kwani serikali inalenga kujua idadi sahihi ya wake kwa ajili ya kuwa na mipango sahihi ya maendeleo” alisisitiza Mkirikiti.

Kwa upande wake Mchungaji Emmanuel Sikazwe ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Amani Mkoa wa Rukwa aliomba kuwepo na utaratibu mzuri wa kufikisha taarifa kuhusu sensa kwa wananchi ili kujenga uelewa mzuri hatua itakayoongeza tija kwenye zoezi la sensa.

Naye Katibu wa Bakwata Mkoa wa Rukwa Ustadh Mohamed Adam alishauri serikali kutoa nafasi ya kutosha kwa viongozi wa madhehebu ya dini kupata elimu ya kina kuhusu sensa ili wapate uelewa wa kuhamasisha jamii kujitokeza kushiriki kikamilifu kuhesabiwa ifikapo Agosti 23 mwaka huu.

“Tunahitaji muda wataalam watupe elimu ya nini maana ya sensa kwani hadi muda huu bado ujumbe wa sensa haujafahamika vizuri katika jamii yetu” alisema Ustadh Adam.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mratibu wa Sensa Mkoa wa Rukwa Adam Ramadhan alisema tayari maeneo ya kuhesabia watu (EAs) 2,190 katika halmashauri zote nne za Rukwa yametengwa pamoja kazi ya kusambaza viperushi imefanyika.

Ramadhan alitaja idadi ya maeneo ya kuhesabia watu kwa kila halmashauri yaliyoandaliwa kuwa Sumbawanga Vijijini (494), Manispaa ya Sumbawanga (534), Kalambo (422) na Nkasi (740).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!