Home Kitaifa MPANGO WA UCHUMI WA BULUU WAIMARISHA FAIDA KWA TANZANIA

MPANGO WA UCHUMI WA BULUU WAIMARISHA FAIDA KWA TANZANIA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za uchumi wa buluu unaweka misingi imara ya kuinufaisha Tanzania kutokana na sekta hiyo.

Amesema hayo wakati akiongoza kikao cha Kamati ya Mawaziri wa sekta zenye mnasaba wa masuala ya uchumi wa buluu cha kupokea taarifa ya utekelezaji na mpango kazi wa sekta hiyo kilichofanyika jijini Dodoma Aprili 16, 2026.

Mhandisi Masauni alisema Tanzania ina fursa nyingi kupitia sekta hiyo ambazo zinaweza kuwanufaisha wananchi kwa kuwawezesha kujipatia ajira kwa kufanya shughuli za kuingiza kipato na hivyo kuchangia uchumi wa nchi.

Aliwaomba mawaziri wote kuungana kwa pamoja na kushirikiana kupitia wataalamu waliopo katika wizara zao zenye mnasaba wa uchumi wa buluu kushiriki katika kuufanyia kazi mpango kazi huo ili uwe endelevu.

“Sisi Ofisi ya Makamu wa Rais ni waratibu na wenye sekta ni ninyi mawaziri kupitia wizara zenu, hivyo tunaomba ushirikiano wenu ili kupata wataalamu kutoka sekta mbalimbali ili kuufanya mpango huu uweze kuwa na tija madhubuti,” alisisitiza Masauni.

Wakichangia wakati wa kikao hicho mara baada ya mawasilisho kuhusu utekelezaji na mpango kazi jumuishi wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu, mawaziri walishauri itolewe zaidi elimu kuhusu sekta hiyo na fursa zilizomo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, walishauri mpango huo ushirikishe wadau mbalimbali.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Dkt. Festo Dugange, alisema ni muhimu kuhusisha ngazi za chini katika kutekeleza shughuli mbalimbali za uchumi wa buluu.

Alisema katika ngazi za Serikali za Mitaa kuna wadau wakiwemo maafisa uvuvi na maliasili ambao wanaweza kushirikishwa na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia maafisa viungo.

Naye Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew, alisisitiza uimarishaji wa uratibu wa sekta ili kuhakikisha matumizi ya rasilimali za maji yanafanyika bila kusababisha migongano ya kimatumizi.

Awali, akitoa neno la utangulizi, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, alisema kuandaa mpango huo kutasaidia kuwa na uelekeo wa kutumia uchumi wa buluu kwa uhakika na kwa manufaa kama ambavyo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inavyoeleza.

Dkt. Muyungi alibainisha kuwa baada ya kuunda kitengo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais kuna mambo mengi ambayo yamefanyika na yatakayofanyika.

Alisema kupitia kikao cha makatibu wakuu, mambo matatu yalizingatiwa ambayo ni utekelezaji wa shughuli za taasisi na idara kwa miezi sita, mambo ya msingi kwa mwaka ujao kwa maana ya uratibu na shughuli zake, pamoja na mengineyo.

Katika kikao hicho, mawaziri walipokea na kupitisha taarifa ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uchumi wa Buluu kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025, mpango kazi wa utekelezaji wa shughuli za uchumi wa buluu kwa mwaka 2026/27, na mpango kazi wa uandaaji wa Mpango wa Matumizi ya Maeneo ya Maji (2025–2030).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!