Home Kitaifa TBS WAKUTANA NA WAZALISHAJI , WAINGIZAJI NA WASAMBAZAJI WA BIDHAA ZA VIPODOZI...

TBS WAKUTANA NA WAZALISHAJI , WAINGIZAJI NA WASAMBAZAJI WA BIDHAA ZA VIPODOZI NCHINI.

Na Mwandishi Wetu.

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limekutana na wadau wa sekta ya vipodozi nchini kwa lengo la kutoa elimu kuhusu matakwa ya viwango, ubora na usalama wa bidhaa hizo zinazotumika kwa kiasi kikubwa na Watanzania.

Mkutano huo uliwakutanisha waagizaji, wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa vipodozi, pamoja na wadau wengine wanaohusika katika mnyororo wa bidhaa hizo, ukiwa na lengo la kuwajengea uelewa kuhusu taratibu na matakwa wanayopaswa kuzingatia ili kuhakikisha vipodozi vinavyofika kwa walaji ni salama na vyenye ubora.

Akizungumza katika mkutano huo leo Julai 28, 2026 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, David Ndibalema, amesema shirika hilo limeitisha kikao hicho kwa kuzingatia jukumu lake la kisheria la kuthibitisha ubora na usalama wa bidhaa, ikiwemo vipodozi.

Amesema kwa mujibu wa Sheria ya Viwango, Sura ya 130, TBS ina wajibu wa kusimamia ubora na usalama wa bidhaa zinazoingia nchini na zinazozalishwa ndani ya nchi, hatua inayolenga kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi matakwa ya viwango husika.

“Vipodozi ni bidhaa inayotumiwa na watu wengi kwa ajili ya kutunza ngozi na kuboresha muonekano, lakini bidhaa hizi zinaweza pia kusababisha madhara kwa afya ya binadamu endapo zitakuwa na viambata visivyoruhusiwa au zitatumika bila kuzingatia viwango,” amesema Ndibalema.

Amesema tafiti mbalimbali zimeendelea kubaini baadhi ya viambata vinavyotumika kwenye vipodozi kuwa na madhara kwa afya ya binadamu, hivyo ni muhimu kwa wazalishaji, waagizaji na wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi matakwa ya viwango kabla ya kufika kwa watumiaji.

Aidha Ndibalema amewataka wadau wote wa sekta hiyo kuzingatia sheria, kanuni na viwango vinavyosimamiwa na TBS, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya za watumiaji na kuhakikisha biashara ya vipodozi inafanyika katika mazingira salama.

Kwa upande wake, Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Habakuki Kalebo, amesema mkutano huo umeandaliwa pia kwa lengo la kuwapa wadau elimu kuhusu taratibu wanazopaswa kufuata wanapoingiza, kuzalisha, kusambaza au kuuza vipodozi nchini.

Amesema TBS ipo tayari kusikiliza changamoto zinazowakabili wadau hao na kuzitafutia ufumbuzi ili kuwawezesha kufanya biashara katika mazingira rafiki, huku usalama wa watumiaji ukipewa kipaumbele.

Kalebo amewasisitiza wadau kuhakikisha bidhaa zao zinawasilishwa TBS kwa ajili ya kupimwa na kuthibitishwa ubora na usalama wake kabla ya kuingia sokoni.

Amesema kuzingatia taratibu hizo kutasaidia kupunguza uwezekano wa wafanyabiashara kupata hasara kutokana na bidhaa zao kuharibika au kuchukuliwa hatua kwa kutokidhi matakwa ya kisheria.

“Afya ya wananchi ni msingi wa uchumi, kwa hiyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha bidhaa inayozalishwa, inayoingizwa au inayouzwa nchini ni bora na salama kwa matumizi,” amesema.

Naye Dkt. Andrew Foyi, daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, amesema elimu kuhusu matumizi salama ya vipodozi inapaswa kutolewa mara kwa mara kwa wazalishaji, waagizaji, wasambazaji, wauzaji na watumiaji.

Amesema baadhi ya vipodozi vinaweza kuwa na viambata vyenye madhara endapo havitatumika kwa viwango vinavyotakiwa, akitaja baadhi ya viambata vinavyoweza kuleta madhara kuwa ni hydroquinone, lead na corticosteroids.

Kwa mujibu wa Dkt. Foyi, matumizi ya vipodozi visivyo salama yanaweza kusababisha madhara ya muda mfupi, ikiwemo kuwasha, kupata vipele, kuungua kwa ngozi, kubadilika kwa ngozi na kuvimba.

Amesema matumizi ya muda mrefu ya baadhi ya vipodozi vyenye viambata hatarishi yanaweza kuathiri viungo vya ndani vya mwili, ikiwemo ini na figo, huku baadhi ya madhara yakihusishwa pia na mfumo wa homoni na afya ya uzazi.

Dkt. Foyi amesema vipodozi ni sehemu ya maisha ya kila siku kwa kuwa vinahusisha bidhaa mbalimbali zinazotumiwa mwilini, hivyo ni muhimu kuhakikisha bidhaa hizo zinakidhi viwango na hazina viambata vinavyoweza kuhatarisha afya.



LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!