Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa jimbo la Musoma mjini,Vedastus Mathayo amekabidhi awamu ya pili ya vifaranga vya kuku,chakula na pesa ya dawa kwa vijana kwaajili ya miradi ya ufugaji.
Awali vifaranga 200 vilikabidhiwa kwa vijana wa Kata ya Bweri na Mshikamano ambao wameanza ufugaji huo baada ya kupata mafunzo.
Awamu hii vijana waliokabidhiwa vifaranga ni kutoka Kata ya Rwamlimi ambao pia wamekabidhiwa vifaranga 100,chakula cha kuku na fedha ya dawa huku vijana kutoka Kata ya Buhare,Nyakato na Kitaji watafikiwa awamu hii.
Akikabidhi vifaranga hivyo kwa vijana hao, Katibu wa mbunge Christopher Majala,amesema huo ni utekelezaji wa ahadi ya mbunge kwa vijana.
Amesema ahadi ya mbunge ni kuwawezesha vijana miradi ya kiuchumi ya ufugaji kuku na samaki kwa njia ya vizimba kwenye Kata 16 zilizopo jimboni.
Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa vifaranga hivyo,vijana hao wamemshukuru mbunge wa jimbo la Musoma mjini,Vwdastus Mathayo kwa moyo wake wa kuwasaidia kujiinua kiuchumi.
Wamesema sio mara ya kwanza kuwasaidia kwani alishafanya hivyo kwa kuwawezesha katika shughuli za kambi ya kilimo na baadhi yao waliokuwa wavumilivu walipata mafanikio .
Wamesema watakwenda kusimamia miradi hiyo vizuri kwa kuwa alianza kuwapa elimu ya ufugaji kupitia wataalamu kabla ya kukabidhiwa.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Rwamlimi Mashauri amempongeza mbunge Mathayo kwa kutimiza ahadi take kwa vijana na kuwata kufanya miradi hiyo kuwa endelevu.
Jimbo la Musoma mjini lina jumla ya Kata 16 ambapo hadi sasa vijana kutoka Kata 6 watafikiwa na vifaranga kwaajili ya ufugaji.









