Home Kitaifa NAIBU WAZIRI KWAGILWA AHIMIZA USHIRIKIANO USAFI WA MAZINGIRA

NAIBU WAZIRI KWAGILWA AHIMIZA USHIRIKIANO USAFI WA MAZINGIRA

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa leo Mei 25, 2026 akiongoza zoezi la usafi wa mazingira lililohusisha uokotaji wa taka na kusafisha mifereji ya maji machafu katika eneo la Taifa Road ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitafanyika jijini Dodoma Juni 05, 2026.

….

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa amezitaka halmashauri, taasisi binafsi, mashirika mbalimbali pamoja na wananchi kuendelea kushirikiana na na Serikali katika kuhakikisha maeneo yanakuwa safi na salama. 

Ametoa rai hiyo wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kuongoza zoezi la upandaji miti na usafi wa mazingira jijini Tanga leo Mei 25, 2026 kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani.

Mhe. Kwagilwa alisema kuwa katika suala la usafi wa mazingira sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuwekeza katika teknolojia na mifumo bora ya usimamizi wa taka na urejelezaji ili kupunguza athari za taka kwa mazingira.

Alisisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha mazingira yanakuwa safi kuanzia nyumbani, maeneo ya biashara, taasisi, masoko hadi maeneo ya wazi huku akiwataka wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya mifumo ya ukusanyaji na utupaji wa taka pamoja na kuepuka vitendo vya uchafuzi wa mazingira.

“Mazingira machafu yana athari kubwa kwa afya na uchumi wa jamii. Uwepo wa taka ovyo, mifereji iliyoziba na uchafuzi wa mazingira huchangia kuenea kwa magonjwa mbalimbali ikiwemo kipindupindu, malaria na magonjwa ya mlipuko. Hivyo, shughuli ya leo isiwe ya siku moja tu, bali iwe sehemu ya utamaduni wetu wa kila siku,” alisistiza.

Halikadhalika, Mhe. Kwagilwa alitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa zitokanazo na taka ikiwemo uzoaji na urejelezaji wa taka ili kuzalisha mbolea, vyakula vya mifugo na bidhaa za viwandani. 

Aliwapongeza wadau mbalimbali ambao wamebadilisha changamoto za taka kuwa fursa na kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kurejeleza taka akisema kuwa hatua hiyo inachangia upatikanaji wa ajira, kuongeza kipato na kukuza uchumi kwa wananchi.

Pamoja na jitihada hizo za wadau, Naibu Waziri huyo alisema Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika kupambana na uchafuzi wa mazingira kwa kuandaa na kutekeleza Mwongozo wa Usimamizi wa Taka Ngumu (Punguza, Tumia Tena na Rejeleza) wa Mwaka 2021. 

Aliongeza kuwa sekta binafsi na asasi za kiraia zimeendelea kutekeleza mwongozo huo ambapo baadhi ya viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki vimeungana pamoja katika kutekeleza Mpango wa Wajibu wa Wazalishaji wa Kusimamia Taka zinazotokana na bidhaa za wanzozalisha kwa kuondosha taka hizo kwenye Mazingira.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mkuu wa Wilaya ya Tanga Dadi Kolimba Mhe. Dadi Kolimba alisema mkoa huo umeendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kufanya usafi katika maeneo yao.

Alisema kuwa wananchi wa Jiji la Tanga kila mwisho wa mwezi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali hushiriki zoezi la usafi wa mazingira na kuondoa uchafu unaozalishwa katika mitaa ya jiji hilo.

Pia, Mhe. Kolimba alitumia nafasi hiyo kupongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuratibu shughuli za usafi na uhifadhi wa  mazingira kupitia zoezi la upandaji wa miti hususan kwa kila halmashauri kupanda miti milioni moja na nusu kila mwaka.

Itakumbukwa kwamba kilele cha Siku ya Mazingira kitafanyika jijini Dodoma Juni 05, 2026 na kaulimbiu ni ‘‘Dira 2050, Tuwajibike Kukijanisha Tanzania’’ ikilenga kuhamasisha jamii kushirki kikamilifu katika kuleta mageuzi na kuwajibika katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa leo Mei 25, 2026 akiongoza zoezi la usafi wa mazingira lililohusisha uokotaji wa taka na kusafisha mifereji ya maji machafu katika eneo la Taifa Road ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitafanyika jijini Dodoma Juni 05, 2026.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa lei Mei 25, 2026 akipanda mti aina ya mwembe katika eneo la Shule ya Sekondari ya Ndaoya, Mtaa wa Chongoleani jijini Tanga ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitafanyika jijini Dodoma Juni 05, 2026.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa leo Mei 25, 2026 akizungumza na wananchi katika uwanja wa Tangamaano jijini Tanga mara baada ya zoezi la usafi wa mazingira lililohusisha uokotaji wa taka na kusafisha mifereji ya maji machafu katika eneo la Taifa Road ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitafanyika jijini Dodoma Juni 05, 2026.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Reuben Kwagilwa leo Mei 25, 2026 akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian alipowasili katika Ofisi za Mkuu wa Mkoa kabla ya zoezi la upandaji miti na usafi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kilele chake kitafanyika jijini Dodoma Juni 05, 2026.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!