Katika kuhakikisha wigo wa masoko katika zao la Korosho unatanuka katika mataifa mbalimbali Duniani, Serikali ya Tanzania imeweka mikakati kuhakikisha zao hilo linaendelea kufanya vizuri katika soko la Dunia kwa kuongeza uzalishaji wa tani laki 4 katika msimu ujao wa kilimo.
Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)Revocatus Rashel katika kongamano la siku moja la kukuza soko la zao la korosho lililofanyika leo Julai 21,2023 katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam lililoandaliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na Ubalozi Vietnam.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa nchi ya Tanzania imeweka malengo makubwa katika uzalishaji wa zao hilo na kwamba kwa kushirikiana na Ubalozi wa Vietnam wanatarajia kuzalisha tani laki nne za korosho zilizochakatwa katika msimu ujao wa kilimo lengo likiwa ni kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza tanzania katika viwanda vya ubanguaji korosho na kupata bidhaa zilizochakatwa ili kupanua wigo wa masoko ya nje.
Aidha amesema wao kama Kituo cha Uwekezaji wameshirikiana katika kuandaa Kongamano hilo ambapo wameliandaa katika njia mbili, moja ni wadau wanakuja hapa, na kwa pamoja wanazungumzia maeneo na vivutio mbalimbali vilivyopo kwenye sekta hiyo ya kilimo hasa kwenye kilimo cha Korosho na uongezaji wa thamani wa zao hilo.
“Korosho ni zao la kimkakati kwa sasa, na Tanzania inazalisha kiasi cha tani laki 250 kwa mwaka lakini mkakati uliowekwa na Serikali ni kuongeza uzalishaji wa zao hilo, na sasa tumeweka lengo la kuzalisha hadi tani laki 4 kwa msimu ujao” amesema Rashel.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya korosho Tanzania Francis Alfred amesema kuwa lengo ni kushawishi wawekezaji kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani katika zao hilo hapa nchini ili Tanzania iwe na uwezo wa kuuza korosho katika masoko mengine ya America na ulaya hali itakayosaidia kutengeneza fursa nyingi za ajira.
“Kupitia Kongamano hili la leo tunapata fursa ya kuongea na wenzetu wa Vietnam kwamba pamoja kuwa wao ndio wanunuzi wakubwa wa korosho ghafi lakini tunataka kuwaomba sasa waje kuwekeza viwanda hapa Tanzania vya kubangua korosho badala ya kununua zikiwa ghafi kwenda kubangua kwao, basi wazibangue hapa vivyo kongamano hili lliloandaliwa na Vietnam pamoja na TIC lina maana kubwa sana katika zao la korosho” amesema Alfred.
Kwa upande wake Meneja wa Bandari ya Mtwara Bw.Norbert J.Kalembwe amema kama Mamlaka ya usimamizi wa Bandari wanayo miundombinu ya kutosha kuhudumia shehena hiyo kwa kuwa sasa wamepanua maegesho ya Meli kwa bandari ya Mtwara na Dar es Salaam.
Aidha Bw.Kalembwe amesema mwaka 2020 Serikali ilikamilisha ujenzi wa Gati mpya ambalo linaweza kuhudumia Meli za ukubwa wa tani 65,000 na kuongeza kina cha maji kwenye maeneo ya kuegesha Meli hivyo Bandari ya Mtwara ina uwezo mkubwa wa usafirishaji kwa njia ya maji.