Home Biashara WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA SABABU ZA MKANDARASI KUONGEZA MUDA WA UJENZI KIWANDA CHA...

WAZIRI NDALICHAKO AAGIZA SABABU ZA MKANDARASI KUONGEZA MUDA WA UJENZI KIWANDA CHA SUKARI MKULAZI KUCHUNGUZWA.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, ameiagiza Bodi ya Kiwanda Cha Sukari Cha Mkulazi kuzifuatilia na kuzichambua sababu ambazo zimekuwa zikitolewa na mkandarasi anayejenga Kiwanda cha sukari Mkulazi kushindwa kukamilisha ujenzi wa Kiwanda hicho ndani ya muda.

Mhe. Ndalichako ameeleza mkandarasi huyo kila unapofika muda wa kukamilisha ujenzi hutoa sababu ya kuongezwa muda, wakati Ujenzi wa Kiwanda hicho ulitarajiwa kukamilika mwezi Agosti mwaka huu, lakini mkandarasi ameomba aongezewe muda hadi mwezi Machi mwakani.

Akiongea leo tarehe 21 Julai, 2022 wilayani Kilosa, wakati alipofanya ziara ya kukagua ujenzi huo, amesisitiza kuwa Bodi hiyo kabla ya kumuongezea muda ihakikishe imejiridhisha juu ya Sababu anazotoa .

“Huyu mkandarasi abanwe muda anaoumba upungue hadi mwezi Desemba mwaka huu, tunataka Kiwanda hiki kianze kuzalisha,ili malengo ya serikali ya Uwekezaji huu kupitia Mfuko wa NSSF yaweze kutimia” amesema

Mhe. Ndalichako ameongeza kuwa lengo la serikali inayoongozwa na Mhe.Rais Samia ni kuongeza fursa za ajira na Uwekezaji kwa watanzania kupitia kiwanda hicho.

Katika hatua nyingine; Mhe. Ndalichako ameutembelea Mradi wa machinjio ya Kisasa ya Nguru wilayani Mvomero, Morogoro ambapo amepongeza kwa hatua iliyofikiwa kwa kuwa mradi huo ukianza kufanya kazi utawezesha Kiwanda kuongeza fursa za Ajira , kuongeza thamani ya mazao ya mifugo hivyo watanzania watanufaika.

Amefafanua kuwa Mhe.Rais Samia amekuwa akihamasisha uwekezaji hivyo serikali kupitia PSSSF imefanya Uwekezaji katika Kiwanda hicho kwakuwa kiwanda hicho kitawezesha serikali kupata fedha za kigeni na kukusanya Kodi.

Wakiongea kwa nyakati tofauti , Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda Cha Sukari Cha Mkulazi, Dkt. Hilideltha Msita, amesema Bodi ya Kampuni Hodhi ya Mkulazi wameyapokea maelekezo na watayatekekza Kwa kuupitia Mpango kazi wa mkandarasi ili kuweza kufuatilia Kwa karibu utekelezaji wake ukamilike mwezi Desemba mwaka huu.

Naye, Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa Mfuko wa PSSSF, Fortunatus Magambo amesema Kiwanda Cha Nguru kitakapo anza kufanya kazi kitakuwa kikichinja ngo’mbe 100 Kwa siku na mbuzi 1000 Kwa siku, Ajira za muda mrefu 350, Ajira 2000 zitakazotokana na mnyororo wa thamani.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!