Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amewataka watumishi wa wizara hiyo wafanye kazi kwa kuzingatia matakwa ya Sheria kanuni na miongozo ya Serikali.
Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na watumishi wa Wizara hiyo ikiwa ni mara ya kwanza tangu aapishwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongoza wizara hiyo.
“Hongereni kwa kufanya kazi, mmeifanya Wizara hii ionekane na kufuatiliwa sana hapa nchini, tuendelee kufanya kazi zaidi kutekeleza mipango yote iliyowekwa kwa kasi na viwango” amesema Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Wizara hiyo inaenda kufanya mambo makubwa zaidi ya yaliyofanyika kwakua ina Wataalamu wazuri katika Sekta zake.
Awali akiwasilisha taarifa ya Wizara hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu amesema kuwa Wizara hiyo itaendelea kuwa kinara katika kutoa furaha kwa Watanzania akibainisha kuwa itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi wake ikiwemo kuongeza vitendea kazi na mazingira bora ya kufanya kazi.

Naye Naibu Katibu Mkuu Nicholas Mkapa amesisitiza Kila Idara kuandaa maandiko mradi ambayo yatawasilishwa kwa wadau wa wizara ili kusaidia ukuaji wa sekta hizo ambazo zimekua na mchango mkubwa katika maendeleo kwa taifa.








