Home Kitaifa DAWASA YAANIKA MIKAKATI YA UBORESHAJI WA HUDUMA YA MAJI HALMASHAURI YA CHALINZE

DAWASA YAANIKA MIKAKATI YA UBORESHAJI WA HUDUMA YA MAJI HALMASHAURI YA CHALINZE

Meneja wa Mkoa wa Chalinze wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Boniface Philemon, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha huduma ya maji katika Halmashauri ya Chalinze ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya uhakika.

Mhandisi Philemon ameyasema hayo leo, Juni 23, 2026, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Gumzo Leo kinachorushwa na Redio Chalinze FM 97.5, ambapo alieleza hatua zinazochukuliwa na DAWASA kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali ya Chalinze.

Amesema miongoni mwa mikakati inayotekelezwa ni pamoja na kufungwa kwa pampu mpya za maji, maboresho ya miundombinu ya usambazaji wa maji na kuongeza uwezo wa mfumo wa usambazaji ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wananchi.

Aidha, Mhandisi Philemon amesema maboresho hayo yanalenga kuongeza kiwango cha maji kinachowafikia wananchi wa Chalinze na maeneo ya jirani, huku yakitarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za upatikanaji wa huduma hiyo.

Katika kipindi hicho, wananchi walipata fursa ya kuwasilisha maoni na changamoto zao, zikiwemo ucheleweshaji wa huduma ya maji katika baadhi ya maeneo, tofauti za upatikanaji wa maji kati ya maeneo mbalimbali pamoja na suala la bili za maji.

Akijibu hoja hizo, Mhandisi Philemon amesema DAWASA imeongeza vifaa, vitendea kazi na usafiri kwa mafundi ili kuimarisha huduma za matengenezo na kuhakikisha hitilafu zinazojitokeza zinatatuliwa kwa wakati.

Vilevile, amesema mamlaka hiyo inaendelea kutekeleza miradi ya muda mfupi na muda mrefu ya kuboresha huduma ya maji katika maeneo ya Chalinze, Mlandizi na maeneo mengine yanayohudumiwa na DAWASA.

Kuhusu mawasiliano na wananchi, amewahimiza wateja kuendelea kutoa taarifa za changamoto za huduma ya maji kupitia kituo cha huduma kwa wateja kwa kupiga namba ya bure 181 ili kuwezesha hatua za haraka kuchukuliwa.

Mhandisi Philemon amesisitiza kuwa DAWASA itaendelea kushirikiana na wananchi katika kuboresha huduma ya maji na kuhakikisha changamoto zilizopo zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!