Home Burudani CHAPATI FESTIVAL KUFANYIKA NCHI NZIMA

CHAPATI FESTIVAL KUFANYIKA NCHI NZIMA

Na Boniface Gideon, TANGA

Waandaaji wa mashindano makubwa ya kupika chapati mkoani Tanga maarufu kama ‘CHAPATI FESTIVAL’ msimu wa pili, Tanga Treasure Network pamoja na Azania Group, wametangaza neema kubwa kwa wafanyabiashara wa vyakula, Mama Lishe na Baba Lishe nchini, ambapo Julai 4 mwaka huu mashindano hayo yatazinduliwa katika Viwanja vya Forodhani na kuenea nchi nzima.

Akizungumza leo na waandishi wa habari, msemaji wa mashindano hayo, Shafii Mohamed, alisema mashindano hayo ya kupika chapati msimu wa pili yatazinduliwa Julai 4 jijini Tanga na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Buriani, na kwamba uzinduzi huo utawezesha kuanza kufanyika katika mikoa yote ya Bara na Visiwani.

“Mashindano haya yanaingia msimu wa pili mfululizo, lakini kuanzia msimu huu tunawatangazia Watanzania kuwa mashindano haya yatafanyika nchi nzima, hivyo Mama Lishe na Baba Lishe nchini wajiandae, tutawafikia popote pale walipo,” alisema Shafii.

Shafii aliongeza kuwa sifa na vigezo vya kushiriki mashindano hayo ni lazima mshiriki awe anamiliki kituo cha kazi ya utoaji wa huduma za vyakula ‘mgahawa’, ambapo wataalamu wa vyakula watazunguka kwenye vituo vyao vya kazi kwa ajili ya ukaguzi na watakaokidhi vigezo watafuzu kuingia kwenye mashindano hayo, ambapo kila mkoa utapata mshindi ambaye atajipatia Sh. 1,000,000 pamoja na vifaa.

“Washiriki wote watapatikana kwenye vituo vyao vya kazi ambapo wataalamu wa vyakula watazunguka kwenye vituo vyao, na watakaokidhi vigezo watafuzu kuingia kwenye mashindano haya. Tunalenga kuwainua wafanyabiashara wote wa vyakula kwa sababu wanatoa huduma muhimu kwa jamii, na ukiangalia hakuna mkoa usiopika na kutumia chapati hapa nchini kwetu,” aliongeza Shafii.

Shafii aliwataka wakazi wa Tanga kujitokeza kwa wingi siku ya ufunguzi wa mashindano hayo ili wapate fursa ya kula na kujifunza namna ya kupika chapati bora.

“Nitumie fursa hii kuwakaribisha wakazi wa Tanga, mje mjifunze lakini pia mle chapati bora zaidi hapa nchini kwetu. Tunaamini kila mtu atafurahia kama ilivyokuwa mwaka jana, lakini mwaka huu itakuwa zaidi ya mwaka uliopita,” alisisitiza Shafii.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!