Home Kitaifa SEKTA BINAFSI INAVYOLETA MAPINDUZI KATIKA MCHEZO WA KUOGELEA KWA KUWANOA BURE MAKOCHA...

SEKTA BINAFSI INAVYOLETA MAPINDUZI KATIKA MCHEZO WA KUOGELEA KWA KUWANOA BURE MAKOCHA WAZAWA

Kocha maarufu kutoka Marekani, Austin Pillado ambaye pia ni Naibu Kocha Mkuu wa timu ya kuogelea kutoka Chuo Washington State (katikati) akiwa ameshika bendera ya Tanzania sambamba na Mkurugenzi mkuu na Mwanzilishi wa shule hiyo ya Monti International, Fatma Fernandes (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), David Mwasogye (kulia). Austin amekuja nchini kuongoza kambi ya siku 10 ya mafunzo maalumu ya kuogelea jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu, Dar es salaam

MCHEZO wa kuogelea ni moja ya michezo ambayo kwa zaidi ya asilimia 90 hutegemea sekta binafsi katika kuuinua mchezo huo na kushamirisha hamasa ya vijana kushiriki mchezo huo ambao pia umekuwa mkombozi kwa vijana wengi wa kitanzania.

Katika kuufikisha mchezo huo kwenye ngazi ya ushindani wa kimataifa, mmoja ya wadau binafsi waliojitokeza kuhuisha vipaji vya watanzania ni Shule ya Kimataifa ya Monti iliyopo jijini Dar es Salaam, ambayo imeandaa kambi ya mafunzo ya siku 10 kwa jili ya kuwanoa makocha na vijana wa Tanzania.

Mafunzo hayo yanatolewa na Kocha maarufu kutoka Marekani, Austin Pillado ambaye pia ni Naibu Kocha Mkuu wa timu ya kuogelea kutoka Chuo Washington State. Pia alikuwa sehemu ya benchi la ufundi lililoshinda ubingwa wa mashindano ya juu kabisa ya michezo ya vyuo vikuu nchini Marekani, yanayoandaliwa na National Collegiate Athletic Association (NCAA) mwaka 2024 akiwa na Arizona State University. 

Kocha huyo mwenye uzoefu wa kutosha ndiye anayetarajiwa kuwapa mbinu na maarifa makocha wazawa wa mchezo huu kupitia miundombinu ya kisasa ya uogelejea iliyoandaliwa na Shule ya Kimataifa ya Monti.

Akizungumzia utekelezaji mafunzo hayo yanayofanyika kuanzia Mei 5 hadi 14 mwaka huu,  Mkurugenzi mkuu na Mwanzilishi wa shule hiyo, Fatma Fernandes anasema lengo kuu ni kuinua viwango vya vipaji vya ndani kufikia hadhi ya kimataifa.

“Tunataka kuziba pengo kati ya vipaji vya ndani na viwango vya kimataifa. Kwa kuwaleta makocha wa kiwango cha juu kama Austin, tunawezesha vijana wetu kupata mafunzo na uchambuzi wa kitaalamu sawa na wanariadha bora duniani,” alisema Fernandes.

Anasema kambi hiyo ni ya kwanza katika ukanda huu kutumia teknolojia ya kamera za chini ya maji (underwater cameras) inayotoa mrejesho wa papo kwa papo kuhusu mbinu za waogeleaji. Mbali na mazoezi ya kimwili, washiriki watapata mafunzo ya ziada kuhusu mikakati ya mashindano, lishe bora na mbinu ya “Fifth Stroke” inayohusisha mbinu za uogejeleaji ambazo ni muhimu katika ushindani wa kisasa.

Kwa mujibu wa Fatma, programu hiyo imeundwa kwa kuzingatia mitaala ya vyuo vikuu vya Marekani vinavyoshiriki mashindano ya NCAA, ikilenga kuimarisha stadi za mbinu nne kuu za kuogelea pamoja na kuendeleza uwezo wa uvumilivu na kasi.

“Uwekezaji katika miundombinu ya michezo, ikiwemo bwawa la kisasa la mita 25 la kiwango cha Olimpiki, una lengo la kunufaisha si wanafunzi wa shule hiyo pekee bali pia jamii pana ya Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla

“Kwa sababu tunaamini mpango huu wa mafunzo ya kambi maalumu ya kuogelea unaendana kikamilifu na maono ya uongozi wetu wa kitaifa — kutoka kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kukuza vipaji vya vijana, hadi kwa Waziri Habari, Sanaa na Michezo, Paul Makonda katika kuhakikisha michezo yote inapewa nafasi ya kukua. 

“Sisi Monti International tunaamini kuogelea kunaweza kuwa nguzo muhimu ya michezo Tanzania, na sekta binafsi ina nafasi kubwa ya kuchangia katika kujenga mafanikio hayo,” anasema Fatma.

Aidha, Chama cha Mchezo wa Kuogelea Tanzania (TSA) nacho kimeshiriki kuwasajili makocha wote waza wa mchezo huo ili waweze kushiriki kikamilifu mafunzo hayo bure.

Akizungumzia ujio wa kocha huyo Mmarekani, Mwenyekiti wa TSA, David Mwasogye anasema ujio wake utasaidia kupunguza au kuziba pengo kati ya vipaji vya ndani na viwango vya kimataifa. 

“Kwa kuwaleta makocha wa kiwango cha juu kama Austin, tunawezesha vijana wetu kupata mafunzo na uchambuzi wa kitaalamu sawa na wanariadha bora duniani,” alisema Mwasogye.

“Lengo kubwa kama chama tunashirikiana na wadau kama Monti International School kwa maendeleo ya mchezo huu kwa kuboresha uwezo wa makocha wetu. Tunaamini makocha wakiwa na uwezo wa hali ya juu watatupatia vijana bora wenye uwezo wa kushindana kimataifa.

Aidha, Kocha Austin Pillado mbali na kupongeza utayari wa Watanzania kujifunza na kupokea changamoto mpya, alisema Tanzania ina vipaji vingi lakini vinahitaji kupewa fursa ya kupata mafunzo ya kiwango cha juu cha kushindana kimataifa. 

“Ndiyo maana nimekuja hapa Tanzania kubadilishana uzoefu kutoka kwenye mfumo wa kimataifa wa NCAA, lengo ni kuona watoto na wakufunzi wanapata mafunzo yenye viwango sawa na wanamichezo bora duniani.

Kocha maarufu kutoka Marekani, Austin Pillado ambaye pia ni Naibu Kocha Mkuu wa timu ya kuogelea kutoka Chuo Washington State (katikati) akiwa ameshika bendera ya Tanzania sambamba na Mkurugenzi mkuu na Mwanzilishi wa shule hiyo ya Monti International, Fatma Fernandes (kushoto) na Mwenyekiti wa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), David Mwasogye (kulia). Austin amekuja nchini kuongoza kambi ya siku 10 ya mafunzo maalumu ya kuogelea jijini Dar es Salaam.

Kocha maarufu kutoka Marekani, Austin Pillado ambaye pia ni Naibu Kocha Mkuu wa timu ya kuogelea kutoka Chuo Washington State na Mkurugenzi mkuu na Mwanzilishi wa shule ya Monti International, Fatma Fernandes (kushoto) wakicheza pamoja na wasanii katika mapokezi yake jijini Dar es salaam. Austin amekuja nchini kuongoza kambi ya siku 10 ya mafunzo maalumu ya kuogelea jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!