
Na Boniface Gideon, Tanga
Watumiaji wa vilainishi vya mafuta nchini wametakiwa kuwa waangalifu wanaponunua bidhaa hizo kutokana na uwepo wa bidhaa feki sokoni. Tahadhari hiyo imetolewa na Ofisa Mipango na Uwezeshaji wa Chama cha Mafundi mkoani Tanga, Said Kijiko, ambaye pia ni Mkurugenzi wa SSMC Ltd, wakati wa kongamano la mafundi (CMT Tanga) lililowakutanisha wadau wa maendeleo wa mkoa huo.
Amesema maendeleo ya sayansi na teknolojia yamechangia uwepo wa bidhaa zisizo halali sokoni, hivyo ni muhimu kwa mnunuzi kujiridhisha na kupata maelezo sahihi kuhusu bidhaa kabla ya kuinunua ili kulinda usalama wake na chombo chake.

Ameeleza kuwa jitihada hizo zinaendana na hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo imekuwa ikikamata bidhaa feki sokoni. Aidha, SSMC Ltd imeingia makubaliano na Mogas Tanzania Ltd kwa lengo la kutoa mafunzo kwa mafundi na wadau kuhusu matumizi sahihi ya vilainishi pamoja na utambuzi wa bidhaa halisi.
Kwa upande wake, fundi mabomba Nassoro Khamis Lukeke amesema upungufu wa elimu sahihi miongoni mwa mafundi na watumiaji unachangia uwepo wa bidhaa feki sokoni. Amesisitiza umuhimu wa wazalishaji na wadau kutoa elimu ili kusaidia kupunguza soko la bidhaa zisizo halali.
MWISHO








