Home Kitaifa 85% YA BARABARA KUPITIKA IFIKAPO 2025

85% YA BARABARA KUPITIKA IFIKAPO 2025

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Victor Seff ameeleza kuwa katika Mpango Mkakati wa Pili utakaoanza mwaka 2021 hadi 2026 taasisi yake itatekeleza shughuli zake kwa kuzingatia vipaumbele ilivyoviandaa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dodoma, wakati akielezea utekelezaji wa shughuli za taasisi yake na mwelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/23, Mhandisi Seff ametaja baadhi ya vipaumbele hivyo kuwa ni kuzitunza barabara zilizo katika hali nzuri na hali ya wastani ili kulinda uwekezaji ambao tayari umeshafanyika.

Mpango mwingine ni kuondoa vikwazo kwenye mtandao wa barabara za wilaya ili ziweze kupitika misimu yote pamoja na kupandisha hadhi barabara za udongo kuwa za changarawe au lami kwa kuzingatia vipaumbele vya kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano wa magari katika majiji, manispaa na miji.

Lengo la mpango mkakati wetu wa pili ni kuwa ifikapo 2025/26 asilimia 85 ya mtandao wa barabara za wilaya chini ya TARURA zitakuwa zinapitika kwa misimu yote na nyakati za mvua hapatakuwa na taharuki inayojitokeza sasa kwa maeneo mengi kutofikika”. Amesema Mhandisi Seff.

Amesisitiza kuwa, “Kuanzia mwaka 2021/22 hadi 2026/27 lengo letu ni kuwa mtandao wa barabara za lami utaongezeka kwa km 1,450.75 ikiwa ni kutoka kilometa 2,404.90 hadi kufikia kilometa 3,855.65, barabara za changarawe zitaongezeka kilometa 73,241.57 ikiwa ni kutoka kilometa 29,116.57 hadi kilometa 102,358.14 na madaraja 3,808 yataongezeka kutoka madaraja 2,812 kufikia madaraja 6,620 ambapo fedha zitakazotumika kwenye mpango huu zinakadiriwa kuwa zaidi ya Shilingi trilioni 4.2.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO, Gerson Msigwa amesema kuwa mwelekeo wa Serikali ni kuhakikisha kuna barabara za uhakika katika kipindi chote, cha mvua na jua.

Kazi wanayofanya TARURA ni pamoja na kufungua kwa mawasiliano ya barabara kwa baadhi ya maeneo, kujenga barabara za udongo au za changarawe, lakini mwelekeo wa Serikali ni kuziweka lami,” ameeleza Msigwa.

Aidha, katika kipindi hiki TARURA inatekeleza Mpango Mkakati wake wa Pili wa miaka Mitano ikiwa mwaka huu 2022/23 ni mwaka wa pili wa Mpango Mkakati huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!