Na WAF – DSM
Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameitaka bodi ya wadhamini ya Bohari ya Dawa (MSD) kusimamia Sheri na utaratibu wa bodi hiyo katika utendaji ili kuongeza uboreshaji wa utoaji huduma.
Waziri Ummy amesema hayo leo Julai 25, 2022 wakati akizindua Bodi hiyo itayosimamia Sheria na taratibu za masuala ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi, Jijini Dar es Salaam .
“kuteuliwa kwenu kuwa wajumbe wa Bodi mpya ya Wadhamini ya Bohari ya Dawa ni kielelezo na ushahidi tosha wa uwezo mlio nao, juhudi, heshima, na umahiri wenu katika kulitumikia Taifa letu.” amesema Waziri UmmyÂ
Sambamba na hilo, amewataka wajumbe hao kuonesha uwezo na weledi ndani ya Bodi pamoja na vipaji walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu na kufanya kazi kama timu ya ushindi katika mfumo wa ugavi wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
Aidha, Waziri Ummy amewataka wakarudishe mifumo yote iliyokuwepo awali kama mfumo wa TEHAMA na Car Track ili kuendelea kuhakiki bidhaa zinaposafirishwa mpaka zitapofika eneo husika.
“Ni imani yangu kuwa, wote mtasimamia vema utendaji wa shughuli za Bohari ya Dawa ili kufikia viwango vya ufanisi bora zaidi katika ugavi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi kwa vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za afya hapa nchini.” Amesema.Â
Pia, Waziri Ummy ameitaka bodi hiyo mpya chini ya Mwenyekiti Bi. Slaa wawe wamekamilisha Kujaza nafasi za wakurugenzi hadi ifikapo Septemba 30, 2022 .
Mbali na hayo amesema, MSD imedhamiria kuanzisha viwanda katika makundi mawili, ikiwemo viwanda vitavyojengwa na MSD yenyewe, na vile ambavyo vitajengwa kwa njia ya ubia kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).
Hata hivyo, Waziri Ummy ameelekeza kuzingatia matumizi mazuri ya fedha, Dawa, vifaa tiba na vitendanishi vyenye ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa.
Aliendelea kusisitiza kusimamia, ununuzi unaoendana na thamani ya fedha ili kuepusha MSD kununua bidhaa kwa bei ya juu kuliko bei za soko.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya bohari ya dawa Bi. Rosemary Slaa amewakaribisha wajumbe hao wapya na kuwataka waanze kazi mara moja kwa kufuata sheria na kanuni kama walivyokula viapo.