Home Kitaifa WILAYA YA LUSHOTO YAPOKEA MRADI WA USAMBAZAJI NA UUZAJI WA MITUNGI YA...

WILAYA YA LUSHOTO YAPOKEA MRADI WA USAMBAZAJI NA UUZAJI WA MITUNGI YA GESI KWA BEI YA RUZUKU

Wananchi wa Wilaya ya Lushoto wamepata fursa mpya ya kunufaika na nishati safi ya kupikia baada ya wilaya hiyo kupokea rasmi mradi wa usambazaji na uuzaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Mradi huo umepokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mheshimiwa Zephania Sumaye, kwa niaba ya wananchi wa wilaya hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia Watanzania wengi zaidi.

Hafla ya mapokezi ya mradi huo imefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Lushoto na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, maafisa kutoka REA pamoja na wawakilishi wa kampuni ya Manjis Logistics Limited, ambayo imepewa jukumu la kutekeleza mradi huo kwa kushirikiana na REA.

Mradi huo ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa na REA nchini kwa lengo la kuharakisha upatikanaji wa nishati safi na salama kwa wananchi, kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Msimamizi wa Mradi kutoka REA, ndugu Abdulrazack Mkomi, alisema kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia unaolenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Alieleza kuwa kupitia mradi huo, REA kwa kushirikiana na Manjis Logistics Limited itasambaza jumla ya mitungi 3,255 ya gesi ya kilo sita kwa wananchi wa Wilaya ya Lushoto kwa bei ya ruzuku ya shilingi 17,500 kwa kila mtungi. Aliongeza kuwa wanufaika wa mpango huo watatakiwa kuwa na Kitambulisho cha Taifa (NIDA) ili kuwezesha utambuzi wa walengwa na kuhakikisha uwazi pamoja na usimamizi bora wa zoezi hilo.

“Madhumuni makubwa ya mradi huu ni kuwapa wananchi fursa ya kupata nishati safi kwa gharama nafuu, kuboresha afya zao na kupunguza athari zinazotokana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira,” alisema Mkomi.

Akizungumza baada ya kupokea mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Mheshimiwa Zephania Sumaye, alimshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuipa kipaumbele ajenda ya nishati safi ya kupikia na kuidhinisha rasilimali zinazowezesha utekelezaji wa miradi inayowanufaisha wananchi moja kwa moja.

Mheshimiwa Sumaye alisema kuwa mradi huo utakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha maisha ya wananchi wa Lushoto kwa kupunguza gharama za upishi, kuimarisha afya za familia na kulinda mazingira. Alibainisha kuwa wanawake na watoto ni miongoni mwa makundi yatakayonufaika zaidi kutokana na kupungua kwa matumizi ya kuni na mkaa, ambayo kwa muda mrefu yamekuwa chanzo cha changamoto mbalimbali za kiafya na kimazingira.

Aidha, aliipongeza REA kwa juhudi zake za kuendelea kubuni na kusimamia miradi ya nishati safi inayolenga kuwafikia wananchi wa vijijini na mijini kwa usawa. Alisema mafanikio ya miradi hiyo yanaonyesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi katika maeneo yote ya nchi.

Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wananchi wa Lushoto kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo ya kupata mitungi ya gesi kwa bei ya ruzuku, akisisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ni hatua muhimu katika kuboresha ustawi wa familia na kulinda mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Mradi huo unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa katika sekta ya matumizi ya nishati ya kupikia katika Wilaya ya Lushoto, huku ukichangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya kuongeza matumizi ya nishati safi, kuboresha afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuimarisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!