Home Kitaifa MADEREVA WASISITIZWA USAFIRISHAJI SALAMA WA KEMIKALI

MADEREVA WASISITIZWA USAFIRISHAJI SALAMA WA KEMIKALI

 Na Okello Thomas

Madereva wanaosafirisha makaa ya mawe nchini wamehimizwa kuzingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia usafirishaji wa kemikali na bidhaa hatarishi ili kulinda usalama wa wananchi, mazingira na mali, sambamba na kuhakikisha shughuli za usafirishaji zinafanyika kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa.

Wito huo umetolewa leo na Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Kanda ya Kusini, Dkt. Hadija Mwema wakati akifungua mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali yaliyowahusisha madereva wa malori yanayosafirisha makaa yamawe wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja alisema kuwa pamoja na makaa ya mawe kuwa bidhaa muhimu katika shughuli za kiuchumi, usafirishaji wake unapaswa kufanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni za Usimamizi na Udhibiti wa kemikali ilikuzuia ajali, uchafuzi wa mazingira na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wausafirishaji.

Alieleza kuwa madereva wanapaswa kuhakikisha magari wanayotumia yapo katika hali nzuri, mizigo imefungwa na kuhifadhiwa kwa usalama, pamoja na kuwa na nyaraka zote muhimu zinazotakiwa kisheria kabla ya kuanza safari.

“Kuzingatia sheria na kanuni si jambo la hiari.Ni wajibu wa kila dereva na mmiliki wa chombo cha usafiri kuhakikisha usafirishaji wa bidhaa unafanyika kwa usalama ilikulinda maisha ya watu, mazingira na mali. Elimu mnayoipata leo inapaswa kuwa sehemu ya utendaji wenu wa kila siku,” alisema Dkt. Hadija.

Aidha, aliwataka madereva kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kutoa taarifa pale wanapobaini changamoto zozote zinazoweza kuhatarisha usalama wakati wa usafirishaji wa bidhaa zinazohitaji uangalizi maalumu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Zubery Maunganya alisema ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali umeendelea kuleta matokeo chanya katika kuimarisha usalama wa usafirishaji wa kemikali na bidhaa nyingine zinazoweza kusababisha madhara endapo hazitasafirishwa kwa kuzingatia sheria.

Alifafanua kuwa taasisi hizo mbili zimekuwa zikishirikiana katika kutoa elimu, kufanya ukaguzi wa magari, kuendesha oparesheni mbalimbali pamoja na kuwajengea uwezo madereva kuhusu wajibu wao wanapokuwa barabarani.

“Lengo letu ni kuona ajali zinazohusisha usafirishaji wa kemikali na bidhaa hatarishi zinapungua. Tunatoa wito kwa madereva wote kufuata sheria za usalama barabarani, kuheshimu alama za barabarani, kuepuka mwendo kasi, kutobeba mizigo kupita kiwango kinachoruhusiwa na kuhakikisha magari yao yanakuwa katika hali nzuri wakatiwote,” alisema.

Baadhi ya madereva walioshiriki mafunzo hayo walisema elimu waliyoipata imewaongezea uelewa kuhusu wajibu wao katika usafirishaji salama wa kemikali nabidhaa nyingine zinazoweza kuleta madhara kwa jamii na mazingira. Walisema wamejifunza mambo mengi ambayo hawakuwa wanayafahamu kwa kina.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!