
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) leo, tarehe 08 Juni 2026, imezindua Mfumo wa Kielektroniki wa Kuoanisha Miamala (Electronic Matching System – EMS) katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni (Interbank Foreign Exchange Market -(IFEM) ambao utawawezesha washiriki wa soko hilo kuwasilisha, kuoanisha na kufanya miamala ya fedha za kigeni kwa njia ya kielektroniki.
Washiriki wa mfumo huu ni mabenki ya biashara na wauzaji wakubwa wa bidhaa nje ya nchi(large exporters) watakaoidhinishwa na BoT kushiriki katika soko kupitia mfumo huu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Naibu Gavana wa BoT anayesimamia Sera za Uchumi naFedha, Dkt. Yamungu Kayanda bila, alisema mfumo huo unaoendeshwa kwa kuzingatia kanunina taratibu zilizowekwa na kusimamiwa na BoT utaongeza uwazi na ufanisi katika upatikanaji wa viwango vya kubadilisha fedha za kigeni.
“Kupitia mfumo huu, tunatarajia kuongezeka kwa uwazi wa soko na kuchochea ufanisi katika upatikanaji wa viwango vya kubadilisha fedha. Aidha, tunategemea kuongezeka kwa ukwasi, kuimarisha ushindani, na kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa soko”.
Aliongeza kuwa mfumo wa EMS utaimarisha uwezo wa Benki Kuu katika ufuatiliaji washughuli za soko na kusaidia kuhakikisha kuwa soko la fedha za kigeni linaendelea kufanya kazi kwa utulivu, ufanisi na kwa kuzingatia viwango bora vya kimataifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha, Bw. Emmanuel Akaro alieleza kuwa kupitia mfumo huu, washiriki watafanya biashara ya fedha za kigeni kwa mfumo wa kutotambulika (anonymous trading), ambapo oda za ununuzi na uuzaji zitaoanishwa moja kwa moja kwa kuzingatia kigezo cha bei na muda wa kuwasilishwa kwa oda husika (price-time priority)
Alisisitiza kuwa mfumo huu utatumika mahsusi kwa utekelezaji wa miamala ya fedha za kigeni ya papo kwa papo (spot transactions) kati ya Shilingi ya Tanzania (TZS) na Dola ya Marekani(USD).
Soko la fedha za kigeni hapa nchini limekuwa na mafanikio makubwa tangu kutungwa kwa Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992.
Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kutungwa kwa Sera ya Ushiriki wa Benki Kuu katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni ya 2023 iliyolenga kuweka mfumo wa ushiriki wa Benki Kuu katika soko na kuimarisha utulivu wa shughuli za ubadilishaji wa fedha za kigeni.
Pia, Kanuni za Maadili ya Soko la Jumla la Fedha za Kigeni za mwaka 2024, zilizojumuisha kanuni 52 zinazotambuliwa kimataifa. Kanuni hizi zinalenga kuimarisha uwazi, uadilifu, weledi na uzingatiaji wa viwango bora vya kimataifa katika shughuli za soko la fedha za kigeni nchini.









