Home Kitaifa TOHASA YAJA NA KAMPENI KUWA MAKINI OKOA MAISHA KWA MADEREVA BODABODA

TOHASA YAJA NA KAMPENI KUWA MAKINI OKOA MAISHA KWA MADEREVA BODABODA

Na Mwandishi Wetu

KAMPENI maalum ya “Kuwa Makini Okoa Maisha” kwa madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda imeanza rasmi mkoani Dar es Salaam, ikiwa na lengo la kuwapatia elimu ya usalama barabarani pamoja na vifaa kinga ili kuchangia kupunguza ajali na vifo vinavyotokana na ajali za barabarani.

Kampeni hiyo imezinduliwa leo Julai 25, 2026, katika eneo la Tangi Bovu-Kawe, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, na  Chama cha Watalaam wa Afya na Usalama Mahala Pa kazi Tanzania(TOHASA), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, OSHA, WCF, SAFETY AND SECURITY, JAFFERJEE na TMHS GROUP .

Akizungumza na madereva wa bodaboda katika eneo hilo, Rais wa TOHASA, Caroline Baraza, amesema wameamua kuanzisha kampeni hiyo kutokana na umuhimu wa kuongeza uelewa wa madereva kuhusu sheria na taratibu za usalama barabarani, hatua ambayo itasaidia kupunguza ajali.

Amesema takwimu za ajali zinaonesha kuwa baadhi ya matukio yanaweza kuzuilika iwapo watumiaji wa barabara watakuwa na elimu ya kutosha na kuzingatia sheria.

“Lengo ni kuwapatia elimu maofisa usafirishaji ili wawe makini na kuheshimu sheria, kwa sababu tunaangalia ajali nyingi zinazotokea na takwimu zinaonesha watu wengi wanakosa elimu na kutokujua wafanye nini wakati gani. Lengo kuu ni kuokoa maisha, ndiyo maana kwenye reflecta zetu tumeandika ‘Kuwa Makini Okoa Maisha’, ambayo ndiyo kaulimbiu yetu,” amesema Baraza.

Aidha, amewataka madereva hao kuzingatia sheria za barabarani na kuwa tayari kuwaelimisha wenzao pale wanapoona wakifanya makosa yanayoweza kuhatarisha usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.

Amesema TOHASA inajumuisha wataalamu kutoka hospitali na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma kwa watu wanaopata dharura, hivyo wana wajibu wa kushiriki katika kampeni zinazolenga kuzuia ajali na kuokoa maisha.

Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Polisi Kawe/Mbweni, Mkoa wa Kinondoni, Adrian Kamara, amesema Jeshi la Polisi limeendelea kushirikiana na TOHASA kutoa elimu kwa madereva wa pikipiki kuhusu matumizi sahihi ya barabara na namna ya kujilinda wao pamoja na abiria.

“Tumeshirikiana na TOHASA ambao wanahusika na usalama mahali pa kazi kuwakumbusha madereva wa pikipiki kuzingatia usalama wao na abiria pamoja na matumizi sahihi ya barabara. Watii sheria za usalama barabarani kwa maana ya kuheshimu vivuko na kutokuendesha pembeni ya barabara,” amesema Kamara.

Amesema madereva wa pikipiki ni watumiaji rasmi wa barabara na wanatambulika kisheria, hivyo wanapaswa kutumia barabara kwa usahihi kama ilivyo kwa magari.

“Tumewafahamisha wao ni watumiaji rasmi na wanatambulika kisheria, hivyo waendeshe pikipiki zao katikati ambako ni sehemu sahihi, kama ni kushoto au kulia wafuate utaratibu kama magari yanavyotembea. Dereva makini hawezi kumparamia mwendesha pikipiki,” amesema.

Kamara pia amesisitiza umuhimu wa madereva kuvaa viakisi mwanga (reflecta) ili waweze kuonekana kwa urahisi wakati wa usiku au katika maeneo yenye mwonekano hafifu.

Aidha, amewakumbusha umuhimu wa kuvaa kofia ngumu wakati wote wanapoendesha pikipiki bila kujali umri, huku TOHASA ikiwapatia baadhi yao reflecta pamoja na miwani ya kujikinga dhidi ya vumbi.

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa TOHASA, Gerald Mrema, amesema wameamua kuanzisha kampeni hiyo kutokana na ongezeko la vifo, majeruhi na ulemavu wa kudumu unaosababishwa na ajali za barabarani.

Mrema amesema taasisi hiyo, kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi nyingine zinazotoa vifaa kinga vya usalama mahali pa kazi, imelenga kuhakikisha madereva hao wanapata elimu na vifaa vinavyoweza kuwakinga dhidi ya madhara yanayoweza kutokea wanapokuwa kazini.

“Taasisi yetu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi pamoja na taasisi mbalimbali ambazo zinatoa vifaa kinga vya usalama mahali pa kazi tumetoa elimu kwa bodaboda tukiwa na kusudi kubwa kwamba baada ya elimu hii watahakikisha wanaendesha vyombo vya moto kwa kuzingatia sheria na taratibu za nchi, kwa kufuata alama za barabarani na kutopakia abiria zaidi ya mmoja,” amesema Mrema.

Amesisitiza umuhimu wa madereva wa bodaboda kutumia vifaa kinga wanapokuwa kazini, ikiwemo reflecta ili waweze kuonekana kwa urahisi na watumiaji wengine wa barabara.

Pia amewataka kuvaa viatu kinga ambavyo vinaweza kusaidia kulinda miguu endapo ajali itatokea, sambamba na kufanya ukaguzi wa pikipiki zao mara kwa mara, hususan kabla ya kuanza safari, ili kuhakikisha vyombo hivyo viko katika hali salama kwa matumizi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tangi Bovu, Athuman Kitunguu, amesema wanashukuru kwa elimu na vifaa kinga walivyopatiwa, akieleza kuwa eneo hilo limekuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani.

Amesema elimu inayotolewa na Jeshi la Polisi imeongeza uelewa miongoni mwa madereva kuhusu umuhimu wa kufuata sheria za usalama barabarani.

“Kwasasa tunashukuru Jeshi la Polisi limekuwa linatupa ushirikiano mzuri na elimu ambazo tunapatiwa zinatuongezea uelewa kuhusu kufuata sheria za usalama barabarani,” amesema Kitunguu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!