Home Kimataifa WANADIASPORA KUWENI MABALOZI WA KUITANGAZA TANZANIA – WAZIRI MKUU

WANADIASPORA KUWENI MABALOZI WA KUITANGAZA TANZANIA – WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wana-Diaspora wote wawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania kokote waliko na wawe tayari kuainisha fursa zilizopo nchini.

Ninyi ni mabalozi wetu, itangazeni Tanzania na onesheni fursa zilizopo nchini ili tupate wawekezaji mahiri wenye mitaji ya kuja kuwekeza nyumbani,” amesema.

Waziri Mkuu ambaye yuko Tokyo, Japan akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa wito huo leo (Jumatano, Septemba 28, 2022) alipokutana na wanachama wa Tanzanite ambayo ni Jumuiya ya Watanzania waishio Japan kwenye hoteli ya Ana Intercontinental jijini humo. Jumuiya hiyo ina wanachama ambao ni wafanyakazi, waliojiajiri na wanafunzi.

Amewataka watambue fursa zilizopo nchini na kuzisemea vizuri ili iwe fursa ya kupata wawekezaji ambao watakuja kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na ikibidi wafanye ubia na Watanzania.

Wana-Diaspora tafuteni marafiki wa kwenda kuwekeza nyumbani kwenye sekta mbalimbali kama utalii, madini, viwanda. Tunawategemea ninyi katika kupata hawa wawekezaji ambao ni makini kwa sababu ninyi mnaishi nao, mnawajua zaidi,” amesema.

Amewataka pia watumie Kiswahili kama njia ya kukuza ajira kwani nchi nyingine zimeona fursa hiyo na zimeamua kukiweka kwenye mitaala yao (syllabus).

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza mafanikio yaliyofikiwa na Serikali ya awamu ya sita ikiwemo uboreshaji katika sekta za elimu, afya, maji, nishati, usafiri na usafirishaji na miundombinu ya barabara na reli.

Kwenye sekta ya afya, tumejenga zaidi ya vituo vya afya 670 ambavyo vina vyumba vya upasuaji, maabara, jengo la mama na mtoto, sehemu ya kutolea dawa na chumba cha kuhifadhia maiti. Katika kila Halmashauri tumejenga hospitali, kila mkoa kuna hospitali na sasa hivi zipo pia hospitali za kanda ambazo zinatoa huduma za kibingwa.”

Akitoa mfano kwenye sekta ya maji, Waziri Mkuu amesema ili kuhakikisha huduma ya majisafi inawafikia wananchi, Serikali imejenga miradi mikubwa ya maji katika miji ya Bunda, Butiama, Bukoba, Tarime, Rorya ambayo yote inatumia maji ya Ziwa Victoria.

Mradi mwingine wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda miji ya Nzega, Tabora na Igunga wenye thamani ya shilingi ya shilingi bilioni 550 unaendelea vizuri. Pia tunao mradi wa maji wa miji 28 kwa ufadhili kutoka Benki ya Exim ya India, hii ni kwa sababu Mheshimiwa Rais Samia tangu akiwa Makamu wa Rais alianzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani na anaiendeleza kwa kasi.

Kuhusu barabara, Waziri Mkuu amesema Serikali imekamilisha barabara kuu za kuunganisha mikoa isipokuwa barabara mbili tu. “Tunaendelea kuunganisha wilaya kwa wilaya na tumeanzisha TARURA ili kuimarisha barabara za vijijini ambapo kwenye kila makao makuu ya wilaya wanapatiwa kilometa mbili za barabara ya lami.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!