Home Kitaifa WAKAZI WA TARAFA YA LIGANGA-LUDEWA WAPATA KITUO CHA AFYA.

WAKAZI WA TARAFA YA LIGANGA-LUDEWA WAPATA KITUO CHA AFYA.

Hatimaye wananchi wa tarafa ya Liganga Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wameondokana na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya waliyokuwa wakikabiliana nayo hapo awali baada ya ujenzi wa kituo cha afya kilichokuwa kikijengwa katika kata ya Mundindi kukamilika kwa asilimia 99.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa kituo hicho katika uzinduzi wa uanzishaji wa huduma kituoni hapo Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi Bwana. Benedict Mhagama amesema hatua hiyo ya ujenzi imefikiwa kwa michango ya Wananchi, Mbunge na Halmashauri kwa kiasi cha sh. Ml. 89 huku Serikali kuu ikitoa fedha za tozo kiasi cha sh. Ml. 500.

“Awamu ya kwanza Rais Samia alituletea kiasi cha sh. Ml. 250 ambazo zilitumika kwa ujenzi wa jengo la OPD, Maabara, kichomea taka na nyumba ya watumishi ambapo majengo yote hayo kwa sasa yamekamilika kwa asilimia 99 na awamu ya pili alituletea Ml. 250 nyingine kwaajili ya jengo la huduma ya mama na watoto, upasuaji, pamoja na jengo la kufulia ambayo kwasasa yamefikia hatua ya kuezeka”. Amesema Mhagama.

Naye mwenyekiti wa Halmashauri Mhe Wise Mgina ambaye pia ni Diwani wa kata hiyo amemshuku Rais Samia kwa kuwapa fedha za kukamilisha ujenzi huo huku akiwataka watanzania kuacha kulalamikia tozo za simu kwakuwa ndizo zinazoleta maendeleo katika huduma za msingi.

“Mwanzoni tozo zilipoanza watu walikuwa wakilalamika sana, lakini kwa sasa natumai walio wengi wameelewa faida ya tozo” Amesema Wise.

Gerald Usili ni katibu tarafa ya Mawengi, akimuwakilisha mkuu wa wilaya ya Ludewa ameishukuru serikali kuu na kuwataka wauguzi kufanya kazi kwa weledi na kufuata miongozo yao ya kazi.

Amesema Ofisi ya Mkurugenzi kupitia Mganga mkuu inapaswa kuendelea kutuma maombi ya fedha serikali kuu kwajili ya kuongeza majengo mengine ili kuweza kukidhi mahitaji yote ya wagonjwa kama huduma za mionzi, macho, pharmacy, vyumba vya waganga, wodi za wagonjwa pamoja na mochwari.

Aidha kwa upande wake mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Dkt. Stanley Mlay amesema kwa sasa kituo hicho kitakuwa na watumishi kumi na sita ambapo wataendelea kuongezeka kulingana na kukua kwa huduma.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kujenga mazoea ya kupata vipimo pindi wanapohisi kuumwa badala ya kunywa dawa pasipo kujua tatizo la ugonjwa wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!