Home Kitaifa TUTAHAKIKISHA MIRADI INAYOJENGWA INALETA TIJA KWA WANANCHI -MAJALIWA

TUTAHAKIKISHA MIRADI INAYOJENGWA INALETA TIJA KWA WANANCHI -MAJALIWA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Manga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Furaha Mwakafwila, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la huduma za dharura katika hospitali ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida, Julai 15, 2022. Ujenzi wa jengo hilo umegharimu shilingi milioni 300 mpaka sasa.

NA MWANDISHI WETU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inaendelea kusimamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya wananchi inayojengwa katika maeneo yote nchini yakiwemo ya vijijini ili kuhakikisha inaleta tija na kuwawezesha wananchi kupata huduma bora kwa wakati.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona Watanzania wote wanapata huduma zote muhimu za kijamii zikiwemo za elimu, afya, maji, pamoja na miundombinu ya mawasiliano ikiwemo barabara.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai 15, 2022) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Singida inayojengwa katika kata ya Solya, wilayani Manyoni mkoani Singida akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo.

Amesema wananchi waendelee kuiamini Serikali yao ambayo imejipanga kuhakikisha inawatumikia na kuwahudumia bila ya ubaguzi wa aina yoyote. “Watumishi wa umma mnatakiwa kuwatumikia wananchi ipasavyo ili kutumiza malengo ya Serikali.”

Amesema Mheshimiwa Rais Samia  amewekeza zaidi katika ujenzi wa shule za watoto wa kike si kwa sababu hawapendi watoto wa kiume, lengo lake ni kumpunguzia binti majukumu ya nyumbani kwa kumuwezesha kuishi shuleni na kupata muda mwingi wa kujisomea zaidi.

Baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo, Mheshimiwa Majaliwa amekagua mradi wa ujenzi wa jengo la kutolea huduma za dharura katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni lililogharimu shilingi milioni 300.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Bw. Melkizedeck Humbe amesema ujenzi wa shule hiyo unaotekelezwa kwa awamu mbili unatarajia kugharimu shilingi bilioni nne. Amesema shule hiyo itakapokamilika itakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 600.

Amesema hadi sasa tayari wameshapokea shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi huo ambapo kwa sasa wanaendelea na ujenzi wa majengo mbalimbali vikiwemo vyumba vya madarasa, maabara ya fizikia na chumba cha jiografia, jengo la utawala na nyumba za walimu.

“Mbali na kutoa fursa kwa wanafunzi wa mkoa wa Singida kupata elimu, pia itapunguza utoro, na mimba kwa wanafunzi wa kike kwa kuwa ni shule ya bweni. Pia shule hiyo itatoa ajira kwa watumishi wa kada mbalimbali wakiwemo walimu, wapishi, wakutubi na walinzi.”

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa Jengo la huduma za dharura katika hospitali ya wilaya ya manyoni, Julai 15, 2022 mkoani Singida. Ujenzi wa jengo hilo umegharimu shilingi milioni 300 mpaka sasa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!