Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kushirikiana na kampuni za tehama ili kukuza Teknolojia nchini
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga wakati akifungua wiki ya majadiliano ya pamoja baina ya kampuni zinazojishughulisha na masuala ya Tehama ndani ya Zanzibar kuhusu namna bora ya kuandaa sera na miongozo ya kuishauri Serikali juu ya ufanyaji wa kazi zao, katika ukumbi wa Park Hayatt iliyopo Mji Mkongwe Wilaya ya Mjini Unguja
Amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anatekeleza kwa vitendo kuifanya Zanzibar kuwa kitovu cha masuala ya teknolojia barani Afrika hivyo serikali ipo tayari kushirikiana na kampuni za ndani ili kufanikisha adhma hiyo yenye lengo la kurahisisha huduma za kiteknolojia ili kuendana na dhana ya uwekezaji kwa wote.
Waziri Soraga amesema baada ya uzinduzi mfumo wa kiteknolojia wa Silicon Zanzibar wenye makao makuu yake Fumba katika mradi wa CPS zaidi ya makampuni mia mbili yamejitokeza na kuonyesha nia ya kuunga mkono juhudi za serikali wapo tayari kukaa na makampuni hayo ili kuona ni kwa namna gani yanaweza kuingia ubia wa kuunga mkono juhudi hizo
Ameongeza kuwa Zanzibar imejaaliwa vijana wengi wenye vipaji vikubwa vya masuala ya Tehama hivyo endapo vipaji hivyo vikisimamiwa ipasavyo vinaweza kuleta mageuzi makubwa ya kiteknolojia ambayo yatapelekea kufikia malengo yaliyokusudiwa
“Hatuwezi kuibagua Tehama na Uchumi wa Buluu na bado tunatakiwa kuonyesha ushawishi mkubwa katika masuala ya teknlojia na mifumo mbali mbali ikiwemo masula ya kifedha na nawashajihisha nyote kuwenda mbali zaidi katika eneo hilo” alisema Soraga
Kwa upande wake Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar Juma Burhani amesema idara yake itahakikisha inawawezesha vijana kwa kuwapatia mafunzo ya usimamizi wa shughuli zao pamoja na kuwawezesha kimitaji kwa lengo la kuongeza ufanisi na kutimiza malengo yao walitojiwekea
Nao baadhi ya washiriki wa majadiliano hayo wamesema mwisho wa mkutano huo watakuja na mpango mzuri wa kuishauri serikali ili kushirikiana kwa pamoja na wanaamini Zanzibar utakuwa mfano wa kuigwa katika uendeshaji wa shughuli za kimifumo barani Afrika na duniani kwa ujumla.