Home Kitaifa WAZIRI NDALICHAKO: SERIKALI KUJENGA VITUO VITANO VYA KULEA UJUZI WA VIJANA NCHINI

WAZIRI NDALICHAKO: SERIKALI KUJENGA VITUO VITANO VYA KULEA UJUZI WA VIJANA NCHINI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako amesema kwa mwaka wa fedha 2022/23, serikali inatarajia kujenga Vituo Atamizi vya kulea ujuzi wa vijana kwenye kanda tano nchini.

Vituo hivyo, vitatoa fursa kwa vijana kufanya mafunzo kwa vitendo sambamba na kufanya shughuli za uzalishaji mali kwenye vituo hivyo ili waweze kujiingizia kipato kutokana na ujuzi watakao kuwa wameupata kwenye vituo hivyo.

“Kwa mfano ukimaliza mafunzo yako ukitaka kusindika chakula kutakuwa na vifaa ambavyo vinaweza kutumika, na itaongeza fursa kwa vijana hasa wasio na uwezo wa kununua vifaa vya kusindika au kufanya shughuli aliyopata ujuzi,” alisema

Mhe. Ndalichako ameyasema hayo tarehe 19 Julai 2022 wakati akizungumza na wanafunzi wa Vyuo vya ufundi vya Don Bosco na VETA jijini Dodoma ambao wananufaika na Programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayotekelezwa na Ofisi hiyo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan inatekeleza programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ili kuhakikisha watu wasio na ajira ambao wako katika soko la ajira wanawezeshwa kwa kujengewa ujuzi utakao wasaidia kufanya shughuli za kiuchumi na hatimaye kujiajiri, kuajiriwa ama kuajiri wenzao.

Amefafanua kuwa kwa mwaka wa fedha 2022/23 serikali imepanga kuendelea kuongeza wigo wa fursa za ajira kwa kutoa mafunzo ya ujuzi wa uchumi wa bluu kwa maeneo ya maziwa na bahari. Mafunzo hayo yatawezesha katika fani ya ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba, ambapo thamani ya Samaki na dagaa itaongezwa.

Aidha, amesema kupitia programu hiyo katika mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2022, serikali imewezesha jumla ya vijana 30,690 kupata ujuzi,

“Serikali ilitoa fedha na kuwezesha mafunzo kwa vijana 3,600 kupata ujuzi wa kilimo cha kisasa kwa kutumia Vitalu Nyumba, Wahitimu wa elimu ya juu 2,246 wamepata mafunzo ya uzoefu wa kazi (internship), Vijana 2,644 wamerasimishiwa ujuzi wao walioupata nje ya mfumo rasmi wa mafunzo, na Vijana 22,200 wamepata ujuzi katika stadi kupitia mafunzo ya Uanagenzi” amesema Waziri Ndalichako.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, aliwataka vijana hao kuthamini jitihada zinazofanywa na serikali ya kuwakwamua kiuchumi kwa kutoa mafunzo bure ya ujuzi.

Awali, Mkuu wa Chuo cha Ufundi Don Bosco, Padri Boniphace Mchami, pamoja na Mkuu wa chuo cha VETA Mwalimu, Stanslaus Charles, wamesema program hiyo imewawezesha vijana kupata ujuzi wa fani zitakazowasaidia kujiajiri na kuajiriwa.

Wakiongea kwa nyakati tofauti vijana wanaonufaika na program hiyo katika vyuo hivyo, wameishukuru serikali kwa kufadhili wa kutoa mafunzo katika fani tofauti kwa vijana ambao wengi walikuwa majumbani na hawakuwa na shughuli za kuwaingizia kipato.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!