Home Kitaifa SENDIGA: SIJARIDHISHWA NA USIMAMIZI MIRADI YA AFYA KALAMBO

SENDIGA: SIJARIDHISHWA NA USIMAMIZI MIRADI YA AFYA KALAMBO

Sehemu ya majengo ya hospitali ya wilaya ya Kalambo ambayo pamoja na mengine yamegharimu shilingi Bilioni 3 tangu yalipoanza kujenga 2018 lakini hayajakamilika hivyo Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (hayupo pichani) ameagiza viongozi wa wilaya hiyo wajitathmini juu ya utendaji wao
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akisalimiana na mama mwenye mtoto mdogo leo wakati alipokagua ujenzi wa kituo cha afya Kanyezi wilaya ya Kalambo ambapo amewahakikishia kukamilika kituo hicho ndani ya siku 14 zijazo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (katikati) akizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera (kushoto) na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Ibrahim Isaack leo alipotembelea kukagua ujnzi wa hospitali ya wilaya Kalambo na kutoridhishwa na mradi huo kutokamilika kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akijibu maswali ya wananchi wa kijiji cha Matai leo alipofanya ziara ya kukagua miundombinu ya afya ambapo ameagiza halmshauri hiyo kukamilisha vituo vya afya na vianze kutoa huduma

Na. OMM Rukwa

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amemwelekeza  Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Tano Mwera na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Shafii Mpenda kujitafakari  juu ya namna wanavyosimamia miradi ya ujenzi wa vituo vya afya kutokana na kutokamilika kwa wakati .  

Ameagiza hayo   leo (Alhamisi Oktoba 20,2022)  kwa nyakati tofauti alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya sekta ya afya wilaya Kalambo pamoja na kuongea na wananchi kusikiliza kero na shida zao.

Sendiga ametembelea na kukagua vituo vinne ambavyo ni kituo cha afya vya Kanyezi (Milioni 400), Legeza Mwendo (Milioni 700), Mwazye (Milioni 500) na hospitali ya wilaya ya Kalambo (Bilioni 3)  ambavyo kwa pamoja vimeshatumia zaidi ya shilingi Bilioni 4.6 lakini huduma bado hazijaanza kutolewa .

Sijafurahishwa kabisa kuona vituo vya afya vilivyokaa miaka zaidi ya minne kutokamilika wakati serikali imetoa fedha. Tatizo hapa nimebaini ni viongozi na watendaji wangu kutosimamia miradi hii ya wananchi” alisema Sendiga.

Sendiga akiwa kwenye eneo la ujenzi wa hospitali ya wilaya alisema “ Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi lazima mkae chini na kujitafakari wilaya hii ina nini? , Kalambo kuna shida kubwa  miradi haikamiliki kwa wakati. Siwezi kukubali kuona miradi yenu ikikwama” alisema Mkuu huyo wa Mkoa wa Rukwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Sunday  Wambura ilionesha kuwa  kituo cha afya Legeza Mwendo ilianza kujengwa mwaka 2018 ambapo serikali ilitoa shilingi Milioni 700 lakini hadi sasa haijakamilika licha ya kuanza kutoa huduma za wagonjwa wa nje.

Pili, kituo cha afya Kanyezi ujenzi wake ulianza Septemba 2018 ambapo serikali ilitoa shilingi Milioni 400 na sasa ujenzi umefikia asilimia 80 huku ikihitaji shilingi milioni 40 zaidi ili ianze kazi kutoa huduma.

Tatu, kituo cha afya Mwazye ujenzi wake ulianza Novemba 2021 kupitia fedha za tozo za miamala ambapo serikali ilitoa shilingi Milioni 500 na ujenzi ambapo imefikia asilimia 90 hadi sasa.

Mradi wa nne aliokagua Mkuu wa mkoa Sendiga ni wa  ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kalambo iliyopo Matai ambapo shilingi Bilioni Tatu zilitolewa na serikali  lakini hadi sasa  mradi huo haijaanza kutoa huduma huku halmashauri ikihitaji shilingi Milioni 600 zaidi kukamilisha miundombinu.

Naye Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Legeza Mwendo Dkt. Emanuel Matinda alisema changamoto kwenye miradi ya ya afya ni upatikanaji wa fedha za ndani ya halmashauri kukamilisha kazi ndogo kama za mifumo ya maji taka, umeme na jengo la upasuaji ili huduma kwa wananchi zianze kutolewa .

Mkuu wa Mkoa huyo wa Rukwa yuko kwenye ziara ya kikazi kukagua miradi ya sekta ya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao kama inavyoelekezwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwisho.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!