Home Kitaifa RC MGUMBA ATAKA MSAKO MITAANI WATOTO WALIOKATISHA MASOMO

RC MGUMBA ATAKA MSAKO MITAANI WATOTO WALIOKATISHA MASOMO

Na Mwandishi Wetu, TANGA.

Mkuu wa mkoa wa Tanga Omari Mgumba amewaagiza wakurugenzi , wasimamizi wa Elimu kwa kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji kuandaa kikosi kazi maalumu kitakachohusika kuwasaka watoto wanaozurura mitaani na wale waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali kuwarudishia mashuleni na kuwachukulia hatua Kali za kisheria wale wote watakaokaidi agizo hilo.

Mgumba alitoa maagizo hayo wakati akizindua vitabu vya muongozo wa kuboresha elimu kwa mkoa wa Tanga ambapo pia aliwataka wakuu wa wilaya , wakuu wa shule waratibu wa elimu kusimamia vyema utekelezaji wa mpango huo ili kufanikisha na kufikia malengo yaliyowekwa na serikali katika kuboresha sekta ya elimu hapa nchini.

“Maeneo yote ya utawala kuanzia ngazi ya wilaya tarafa, kata, mitaa, vijiji na vitongoji waendelee kuandaa timu za kuwasaka wanafunzi wanaodhurura mitaani na waliokatisha masomo kabla ya kumalizia ngazi yao ya Elimu wakati wanapaswa wawepo mashuleni hii ni pamoja na kuhakikisha watoto wote wenye umri wa kuanza shule wazazi wao wanapelekwa shuleni na watakaokaidi sheria ifuate mkondo wake” alisema Mgumba.

Mgumba aliwataka wazazi walezi na jamii kwa ujumla wenye tabia ya kuwashurtisha watoto wao wasifanye vizuri katika mitihani yao kuachana tabia na dhana hiyo potofu ambayo inalenga kukatisha ndoto zao za baadaye.

“Nimesikia kuna baadhi ya wazazi wanaowafundisha watoto waandike madudu kwenye mitihani yao kwa kisingizio cha kusema elimu ni gharama akifaulu nitatoa pesa nyingi sana huo ni ukatili mkubwa sana kwa watoto wetu tunakatisha ndoto zao naombeni sana tuwaache watoto wasome na waweze kutimiza ndoto zao” aliongeza

Aidha aliwatahadharisha watendaji na wasimamizi wote wa miradi ya elimu ambao wamekuwa wakichangia kwa namna moja ama nyingine isikamilike kwa wakati kuwawajibishwa kisheria ikiwezekana kuwaondoa ndani ya mkoa wa Tanga.

“Nilichojifunza kwa mkoa wa Tanga kwa kipindi kifupi nilichofika hatuna haraka, ipo miradi ya ujenzi wa shule ambazo zililetewa fedha na serikali kwaajili ya kuitekeleza lakini bado haijakamilika, nitoe maelekezo kwa mujibu wa miongozo iliyotolewa na serikali kila mradi unatakiwa ikamilike kwa wakati uliopangwa vinginevyo wahusika tutawachukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuomba wahamishwe”

Awali akizungumza katibu tawala mkoa wa Tanga Pilli Mnyema amesema zipo baadhi ya wilaya ya Tanga bado hazifanyi vizuri kwenye ufaulu wa masomo mbalimbali kwa kuanzia darasa la nne , la Saba. Kidato cha nne na sita Hali ambayo inashusha ufaulu wa mkoa mzima kitaifa hivyo kuwaomba wadau wa Elimu kwa kushirikiana na walimu wa kuu kuongeza jitihada pamoja na kupitia miongozo hiyo ili kuweza kuinua kiwango cha elimu kwa ujumla.

“Tumekuwa tukipata wastani ambao sio mzuri na unasababisha mkoa wa Tanga kwenye ngazi za kitaifa kuwa kwenye changamoto tumefanya tathmini ya kidato cha nne wa mkoa

Kwa upande wake Afisa elimu mkoa wa Tanga Newaho Mkisi aliwataka walimu wa shule zote za serikali na binafsi kutumia vitabu hivyo vyenye miongozo ya kukuza elimu iwe mikakati yao na kiutekelezaji ili kuhakikisha inaleta mabadiliko ya ufaulu kwa wanafunzi wa shule zote zilizopo.

“Kuna mikakati mingi kwaajili ya kuboresha elimu lakini kwa kushirikiana na ofisi ya Rais Tamisemi wametugawia vitabu vingine vya kutusaidia kuongeza ufaulu katika nchi yetu, mkoa wa Tanga tuna shule za msingi 1800 na sekondari 3001 zote hizi sisi walimu tuliopo na viongozi wa kata tunatakiwa tuishi katika hiyo mikakati ili tuweze kuuongezea ufaulu mkoa wetu” alisema Mkisi.

Vitabu hivyo vitatu vya miongozo ya elimu hapa nchini vilizinduliwa rasmi kitaifa na waziri mkuu Kassimu Majaliwa.

MWISHO.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!