Home Kitaifa OPARESHENI KALI KUWASAKA WANAFUNZI AMBAO HAWAJARIPOTI KIDATO CHA KWANZA

OPARESHENI KALI KUWASAKA WANAFUNZI AMBAO HAWAJARIPOTI KIDATO CHA KWANZA

Na Shomari Binda – Musoma

MKUU wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ametoa maagizo kwa wakuu wa Wilaya wote kuanzisha opresheni kali kuwatafuta wanafunzi ambao bado hawajaripoti shuleni kwa kidato cha kwanza mwaka huu.

Agizo hili alilitowa leo, Machi 5, 2025, wakati akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa uwekezaji. Mtambi alieleza kuwa asilimia 83.1 ya wanafunzi wameripoti shuleni, lakini wengine bado hawajafika na hivyo wanahitaji kusakwa ili kuhakikisha wanajiunga na masomo.

Alisema pia kwamba kuna taarifa za baadhi ya wanafunzi kujiingiza katika shughuli za uchimbaji wa madini na wengine kuozeshwa, hasa watoto wa kike. Kanali Mtambi alisisitiza kuwa serikali ya mkoa wa Mara haitavumilia mzazi atakayemzuia mtoto wake kwenda shule kwa namna yoyote, akieleza kuwa elimu ni haki ya kila mtoto. Aliongeza kuwa serikali kuu imewekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi na uboreshaji wa elimu, na hivyo ni muhimu kuhakikisha watoto wote wanajiunga na shule.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alisema kwamba uandikishaji wa wanafunzi kwa elimu ya awali umekaribia asilimia 100, na kwa upande wa elimu ya msingi, uandikishaji umevuka lengo na kufikia asilimia 107.

Mtambi aligusia pia suala la chakula mashuleni, ambapo alisisitiza kila halmashauri kuandaa taarifa ya idadi ya wanafunzi na shule zinazotoa huduma ya chakula. Hali kadhalika, alihimiza umuhimu wa elimu ya awali na huduma za afya kuwa kipaumbele katika bajeti za halmashauri.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa alisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, akitilia mkazo kwa taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kuachana na matumizi ya kuni na kuzingatia nishati safi.

Alimalizia kwa kuhimiza viongozi wote kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni kinara wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!