Home Kitaifa NM-AIST YAWASILISHA ZAIDI YA BUNIFU 20 WIKI YA ELIMU, UJUZI NA UBUNIFU.

NM-AIST YAWASILISHA ZAIDI YA BUNIFU 20 WIKI YA ELIMU, UJUZI NA UBUNIFU.

Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na washiriki wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu inayofanyika jijini Tanga kuhusu bunifu mbalimbali zinazozalishwa na watafiti na wabunifu wanaoshirikiana na taasisi hiyo.

Katika maadhimisho hayo, NM-AIST imewasilisha jumla ya bunifu 20, ambazo nyingi zimetokana na tafiti na kazi za watafiti wa ndani ya taasisi, huku nyingine zikiwa zimezalishwa na wabunifu wa nje wanaopatiwa malezi, mafunzo na mwongozo kupitia taasisi hiyo. Bunifu hizo zinaonesha jitihada za NM-AIST katika kuunganisha utafiti, ubunifu na mahitaji halisi ya jamii.

Aidha, taasisi hiyo imewashirikisha wawakilishi wa vikundi vya wanawake wanaopatiwa msaada na mwongozo katika kuboresha bidhaa zao na kuongeza thamani. Hatua hiyo inalenga kuwawezesha kutumia maarifa na teknolojia kuongeza ubora, tija na ushindani wa bidhaa zao sokoni.

Katika hatua nyingine, NM-AIST imewasilisha kampuni tatu zilizoanzishwa kutokana na bunifu na tafiti zilizofanyika ndani ya taasisi. Kampuni hizo ni Nano Filter, inayojihusisha na teknolojia ya uchujaji wa maji; AfriTech, inayotumia teknolojia inayotokana na mabaki ya korosho katika uchakataji wa ngozi; na Uji Chap Chap, inayolenga kuchangia afya bora kupitia bidhaa za lishe.

Ushiriki wa NM-AIST katika maonyesho hayo unaendelea kutoa fursa kwa wananchi kujifunza namna ambavyo matokeo ya utafiti na ubunifu yanaweza kubadilishwa kuwa bidhaa na huduma zenye manufaa kwa jamii. Aidha, ushiriki huo unaonesha mchango wa taasisi katika kukuza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo muhimu za maendeleo ya Tanzania.

NM-AIST inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuifikia jamii, kuwatamia wajasiriamali na kukuza ubunifu kwa maendeleo endelevu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!