Home Kitaifa MAELFU WAMZIKA MASANCHE, KATAMBI AMLILIA

MAELFU WAMZIKA MASANCHE, KATAMBI AMLILIA

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini, Mheshimiwa Patrobas Katambi ameongoza maelfu ya waombelezaji waliojitokeza katika mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, marehemu Rajab Masanche aliyefariki dunia alfajiri ya Septemba 28, 2022 takribani masaa 12 baada ya kuongoza kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga lililopitia na kujadili Taarifa za Hesabu za Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022

Mazishi hayo yamefanyika katika makaburi ya Nguzonane yaliyopo Mjini Shinyanga na kuhudhuriwa na maelfu ya watu kutoka kila pembe ya Mji wa Shinyanga na Vitongoji vyake.

Katika salamu zake za rambirambi zilizosomwa kwa niaba yake na Katibu wake, Katambi amemuelezea marehemu Masanche kuwa alikuwa ni mtu mchapakazi, mkarimu, mcheshi, hodari na muda wote alipenda kufanya kazi za mwajiri wake kwa ufanisi mkubwa katika kuwahudumia wananchi wa Manispaa ya Shinyanga.

Akiongea katika mazishi hayo, Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Sheikh Ismail Habibu Makusanya, amewataka watu wote kumcha Mwenyezi Mungu na kujiandaa na safari ya mwisho ambayo kila nafsi katika dunia hii itaonja mauti. Sheikh Makusanya amewaomba watu wote kuwapatia haki zao marehemu wanaotangulia mbele za haki ikiwa ni pamoja na haki ya kuwasamehe yale yote waliowakosea enzi za uhai wao kama inavyofundishwa katika mafundisho ya imani ya dini ya Kiislamu.

Marehemu Rajabu Masanche ameacha mjane na atakumbukwa na wengi kwa tabia yake ya kufurahi na mtu tabia ambayo alikuwa nayo wakati wa uhai wake.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!