Mke wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mama Mariam Mwinyi amesema Taasisi ya Zanzibar maisha Bora Foundation itaendelea kuwahamasisha Wazanzibar kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujikinga na maradhi.
Ameyasema hayo leo alipozungumza na wananchi waliojitokeza kushiriki matembezi ya mwisho wa mwezi yalioanzia nje ya ofisi ya Baraza la Manispaa ya Magharibi ‘A’ na kumalizila katika viwanja vya Dole.
Mama Mwinyi amesema ufanyaji wa mazoezi wa mara kwa mara pia husaidia kwa kiasi kikubwa kujenga upendo na umoja.
Akizungumza suala la utoro kwa wanafunzi, Mama Mwinyi amewataka wazazi kuwa na mazoea ya kufika shuleni kufuatilia maendeleo ya watoto wao ili kupunguza hali ya utoro.
Mama Mwinyi amehimiza wanafunzi kutambua umuhimu wa elimu kwa kuwa ni msingi wa maisha.
Akizungumzia suala la chanjo ya UVIKO – 19 Mama Mwinyi amewataka Wazanzibar kujitokeza kwa wingi kuchanjwa.
Naye Waziri wa Habari, Vijana na Michezo Tabia Maulid Mwita amesema Wizara yake itahakikisha inashirikiana kwa ukaribu na Taasisi ya Zanzibar maisha Bora Foundation ili kufikia malengo ya taasisi hiyo.