
▪️ Asema utekelezaji wa Bwawa la Farkwa kuanza baada ya kukamilika kwa taratibu za manunuzi
▪️ Aagiza kukomeshwa kwa ukamataji usio na msingi wa vitendea kazi vya wananchi
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha miradi yote ya maendeleo iliyopungua kasi ya utekelezaji inaanza tena kutekelezwa kwa kasi inayotakiwa ili wananchi waendelee kunufaika na huduma za kijamii na kiuchumi.

Amesema hayo leo Jumapili, Mei 17, 2026, alipowahutubia wananchi wa Wilaya ya Chemba katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kambi ya Nyasa, akiwa katika ziara ya kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi.
Dkt. Mwigulu amesema baadhi ya miradi ilipungua kasi baada ya Serikali kuelekeza nguvu kubwa katika kukamilisha miradi ya kimkakati ya kitaifa iliyokuwa imefikia hatua za mwisho, ikiwemo Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, reli ya kisasa pamoja na Daraja la Kigongo–Busisi.

“Kilichosababisha baadhi ya miradi kupungua kasi haikuwa uzembe wala kupuuza. Ilikuwa ni mkakati wa kukamilisha miradi iliyokuwa imekaribia kukamilika ili ianze kutumika,” amesema.
Amesema Serikali sasa imeweka kipaumbele katika kuhakikisha miradi yote iliyokuwa imepungua kasi inaanza tena kutekelezwa, huku miradi ambayo mikataba yake tayari imesainiwa ikitengewa fedha za kuanza kazi.
Kuhusu Mradi wa Bwawa la Farkwa, Dkt. Mwigulu amesema mradi huo, unaokadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 312, utaanza kutekelezwa mara baada ya kukamilika kwa taratibu za kimanunuzi.
“Tunapoanza bajeti mpya naamini mtakuwa mmeanza kuona mkandarasi akiwa eneo la mradi kutekeleza mradi huo wa kihistoria,” amesema.
Amesema Serikali imeelekeza miradi mipya ya maji ibuniwe kwa namna itakayotoa huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani, mifugo na shughuli za kilimo.
Aidha, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta za afya, elimu, maji na nishati, hatua ambayo imebadili kwa kiwango kikubwa maisha ya wananchi.
Katika sekta ya afya, amesema Serikali imejenga hospitali za wilaya zaidi ya 100, vituo vya afya zaidi ya 600 na zahanati zaidi ya 2,700, sambamba na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa vya uchunguzi katika hospitali za rufaa na za kanda.
Katika sekta ya elimu, amesema Serikali imejenga shule za amali 103, zikiwemo shule 29 za mkondo wa uhandisi, pamoja na kuendelea kuongeza miundombinu ya shule za msingi na sekondari nchini.
Kuhusu nishati, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imejipanga kumaliza changamoto ya kukatika kwa umeme kupitia utekelezaji wa Mradi wa Gridi Imara wenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.1.
“Mkiona umeme unakatika katika baadhi ya maeneo siyo upungufu wa umeme tena. Changamoto ipo kwenye uimara wa gridi kutokana na ongezeko kubwa la matumizi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza viongozi na watendaji kuacha vitendo vya ukamataji usio na msingi pamoja na kushikilia vitendea kazi vya wananchi kwa makosa madogo.
“Haya mambo ya kushikilia vitendea kazi vya wananchi tuachane nayo. Mtu anafanya shughuli yake ya kujitafutia kipato halafu mnachukua kitendea kazi chake; hiyo ni kuua mtaji na maisha ya familia yake,” amesema.
Amesema Serikali itaendelea kulinda haki za wananchi na kuhakikisha sheria hazitumiki kuwaonea wananchi au kuwanyima fursa za kufanya shughuli halali za uzalishaji.
Aidha, amesema Serikali inaendelea na hatua za kuifuta sheria ya kutaifisha mali ambayo imekuwa ikitumika vibaya katika baadhi ya maeneo na kusababisha wananchi kupoteza mali zao isivyo halali.









