Home Kitaifa CMSA YAHIMIZA WANANCHI KUWEKEZA KUPITIA MIFUMO RASMI YA MASOKO YA MITAJI

CMSA YAHIMIZA WANANCHI KUWEKEZA KUPITIA MIFUMO RASMI YA MASOKO YA MITAJI

Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imewahimiza wananchi kutumia mifumo rasmi ya uwekezaji ili kunufaika na fursa zinazotolewa katika soko la mitaji kwa usalama na kwa kuzingatia sheria.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Uhusiano na Elimu kwa Umma wa CMSA, Stella Anastazi, amesema mamlaka hiyo huidhinisha bidhaa na huduma za uwekezaji zinazokidhi vigezo, zikiwemo hisa, hatifungani na mifuko ya uwekezaji wa pamoja, ili kuhakikisha wawekezaji wanafanya uwekezaji katika mazingira salama.

Amesema CMSA pia hutoa leseni mbalimbali kwa wadau wa sekta ya masoko ya mitaji, ikiwemo leseni ya meneja wa mfuko na wakala wa soko la hisa, zinazowawezesha kubuni na kusimamia mifuko ya uwekezaji, kutoa ushauri wa uwekezaji, kufungua akaunti za wawekezaji na kununua au kuuza hisa na hatifungani kwa niaba ya wateja.

Aidha, amesema chini ya sekta hiyo pia kuna Soko la Bidhaa Tanzania, ambalo linaendesha minada ya kidigitali inayowezesha bidhaa mbalimbali, hususan mazao ya wakulima, kuuzwa kwa wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Stella ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda la CMSA katika maonesho yanayoendelea hadi Julai 13 ili kupata elimu kuhusu fursa za uwekezaji, kutatuliwa changamoto zinazowakabili na kupata mwongozo wa namna ya kuwekeza kupitia mifumo rasmi.

Pia amewahimiza wanaotaka kufanya kazi katika sekta ya masoko ya mitaji kufika banda la CMSA ili kupata maelezo kuhusu leseni zinazohitajika na taratibu za kujiunga na sekta hiyo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!