
Na Boniface Gideon, KILINDI
Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga kimenusa upigaji wa vifaa vya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilindi, katika ziara ya Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Tanga iliyofanyika jana ikiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rajab Abdalahman, ambapo ilibaini wizi wa vifaa vya ujenzi wa hospitali hiyo.
Katika taarifa yake kwa umma iliyotangazwa mbele ya mkutano wa hadhara mara baada ya kufanya ukaguzi wa hospitali hiyo, Rajab alisema chama hicho kimebaini wizi wa vifaa, ikiwemo saruji (cement) mifuko zaidi ya 100 ikiibwa, huku mifuko zaidi ya 150 ikiharibika kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila kutumika kama ilivyokusudiwa.
“Ndugu wananchi, hapa tumebaini wizi wa cement na mifuko mingine imeharibika kutokana na kukaa kwa muda mrefu bila kutumika, lakini pia hatujui vifaa vingine kama vile nondo huenda kukawa nako kuna wizi,” aliongeza Rajab.
Rajab alimtaka Mkuu wa Wilaya hiyo kuhakikisha wale wote waliohusika kufanya wizi huo wanachukuliwa hatua za kisheria ili wawajibike kutokana na makosa yao.
“Mkuu wa Wilaya, tunataka uchukue hatua stahiki kwa wahusika wote waliofanya wizi huu. Taarifa hii siyo nzuri kutokana na Serikali kuwekeza fedha nyingi sana kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya afya, halafu watu wachache wanakuja kuhujumu. Hii haikubaliki,” aliongeza Rajab.






