Home Kitaifa SUNGUSUNGU WAONYWA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI

SUNGUSUNGU WAONYWA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI

Viongozi wa vikundi vya ulinzi shirikishi zaidi ya 500 wa kanda ya ziwa, wamepewa elimu ya ulinzi shirikishi juu ya namna ya kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria za nchi huku wakipewa onyo kali kujichukulia sheria mkononi.

Hayo yameelezwa na OCS wa kituo cha Polisi wilaya ya Maswa, Mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Ramadhani Mkimbu katika mkutano wa pili wa viongozi wa sungusungu uliofanyika Agost 30, 2023 eneo la Malampaka wilaya hiyo mkoani Simiyu.

Aidha Mkutano huo uliolenga kuwapa elimu ya pamoja Sungusungu wa kanda ya ziwa umehusisha maafisa wa Jeshi la Polisi kutoka Mkoa wa Mwanza, Shinyanga na Simiyu waliowasilisha mada mbalimbali kwa viongozi wa vikundi hivyo ili kuwapa uelewa wa pamoja kwenye masuala ya sheria na usalama wa wananchi.

Awali Mkimbu aliwaeleza viongozi hao sababu ya kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi shirikishi kuwa ni kuiweka jamii karibu na Jeshi la Polisi ili kutatua changamoto za kihalifu kwenye jamii ambapo uanzishwaji wa vikundi hivyo ni utekelezaji wa moja ya miradi ya Polisi Jamii ambapo amewataka kushirikiana na askari kata kwani wao ni wataalamu wa upelelezi na ukamataji salama.

Aidha, OCS Mkimbu ametoa onyo kali kwa kikundi chochote cha Sungungu kitakacho bainika kuwapiga au kuwalipisha faini watuhumiwa kinyume na sheria, kitawajibishwa kwa mujibu wa sheria kulingana na kosa lililotendeka.

Chombo chenye mamlaka ya kutoa hukumu ni Mahakama pekeyake, wewe Sungusungu mimi Polisi hatuna mamlaka kisheria ya kutoa hukumu kama baadhi yenu mnavyofanya” amasema OCS Mkimbu.

Kwa upande wake Afisa Polisi Jamii Mkoa wa Mwanza Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhani Sarige amewasihi viongozi hao kwenda kuwaelimisha wenzao ili kuwe na muunganiko mzuri kati yao na Jeshi la Polisi.

Nae Mwenyekiti wa vikundi vyote vya Sungusungu kanda ya ziwa Shimbi Regan amekemea baadhi ya watu wanaoviita vikundi vya ulinzi shirikishi Jeshi, “Kuna watu wanapotosha wanawaita Sungungu jeshi, sisi siyo Jeshi ni wasalama ” amesisitiza Regan

Aidha, ameshukuru uongozi wa Jeshi la Polisi kwa kutambua mchango wa sungusungu na kuomba elimu iliyotolewa iwe endelevu ili kuleta uelewa wa pamoja kwenye masuala ya usalama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!