Home Kitaifa WIZARA YA MADINI KUUTANGAZA MGODI WA NYAKAVANGALA KUVUTIA WAWEKEZAJI

WIZARA YA MADINI KUUTANGAZA MGODI WA NYAKAVANGALA KUVUTIA WAWEKEZAJI

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amelitaka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kufanya Utafiti katika eneo la mgodi wa Nyakavangala ili kujua muelekeo wa mwamba na kiwango cha madini yaliyopo katika eneo hilo.

Dkt. Kiruswa ameyasema hayo Juni 17, 2022 alipotembelea mgodi wa Nyakavangala uliyopo katika kata ya Malengamakali Mkoani Iringa.

Aidha, Dkt. Kiruswa amesema Wizara ya Madini itaendelea kufanya jitihada za kulitangaza eneo la mgodi wa dhahabu la Nyakavangala kwa lengo la kuhamasisha uwekezaji katika eneo hilo.

Pia, Dkt. Kiruswa amewataka, wachimbaji wadogo wa Nyakavangala kuzingatia usalama mahala pa kazi ili waweze kuchimba kwa kuzingatia usalama wa watu na mazingira.

Ziara hiyo, imekuja baada ya Mbunge wa Viti Maalumu wa Iringa mjini Dkt. Rita Kabati kuuliza swali Bungeni akitaka kujua ni lini serikali itawasaidia wachimbaji wadogo wa Nyakavangala kufanyiwa utafiti ili kujua kiwango cha madini yaliyopo katika eneo hilo ili wachimbe kwa tija na kuwavutia wawekezaji.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ametumia fursa hiyo kuwataka wachimbaji wadogo wa madini kote nchini kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agositi 23, 2022.

“Naomba nitumie fursa hii kuwaomba wachimbaji na wadau wa Sekta ya Madini kote nchini kujiandaa kuhesabiwa siku ya Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika tarehe 23 Agositi, 2022, ushiriki wako utaisaidia serikali kujua idadi ya wachimbaji kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema Dkt. Kiruswa.

Kwa upande wake, Katibu wa Wamiliki wa Mgodi wa Nyakavangala John Tinanzila amesema mgodi wa Nyakavangala umeweza kuzalisha gramu 9931 za dhahabu katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka Mei 2021 mpaka Mei 2022.

Pia, Tinanzila amemuomba Naibu Waziri kusaidia kupata wawekezaji na taarifa za kijiolojia katika mgodi huo na ameongeza kuwa, nishati ya umeme na maji safi imekuwa ni changamoto kubwa katika mgodi huo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!