Home Kitaifa WIZARA YA ELIMU ITAHAKIKISHA INAGAWA RASILIMALI NA FURSA KWA HAKI-WAZIRI MKENDA

WIZARA YA ELIMU ITAHAKIKISHA INAGAWA RASILIMALI NA FURSA KWA HAKI-WAZIRI MKENDA

Na Mathias Canal, WEST- Bagamoyo, Pwani

Serikali imempongeza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) Bi Bahati Geuzye pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya mamlaka hiyo Prof Maurice Mbago kwa kazi kubwa na nzuri wanayoifanya kwa utoaji wa rasilimali kote nchini na kuitaka kuendelea kutoa fursa kwa haki katika kusaidia na kugawa rasilimali zinazohitajika katika maeneo mbalimbali mchini.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 8 Novemba 2022 wakati akizungumza na wananchi mara baada ya kukabidhiwa nyumba nne za walimu wa shule ya msingi Msinune iliyopo katika Halmashauri ya Chalinze, Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani zilizojengwa na Taasisi ya Flaviana Matata Foundation pamoja na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

Waziri Mkenda ameitaka Mamlaka ya elimu Tanzania (TEA) kuhakikisha kuwa inabainisha vigezo vya kutoa rasilimali na fursa katika jamii kwani uwazi ni jambo la muhimu ili kurahisisha utoaji haki.

“Kwa taasisi zetu zote mnavyo vigezo mnavyovitumia katika ugawaji rasilimali hivyo ni lazima tukae tupitie na kuviboresha ili kubaini maeneo mahususi ya kuvipeleka ili kila mtoto anayezaliwa hapa Tanzania apate fursa sawa” Amekaririwa Waziri Mkenda na kuongeza kuwa

“Fursa zigawanywe sawa sawa na vigezo vitangazwe vya utoaji fursa, hatuwezi kujenga nchi kwa kugawa fursa kwa upendeleo lazima tutoe kwa haki, tatizo uwazi wakati mwingine watu hawapendi lakini lazima tusimamie” Amekaririwa Waziri Mkenda

Prof Mkenda amesema kuwa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliijenga nchi ya Tanzania kwa usawa wa binadamu, na usawa huo utekelezaji wake ni kujifunza hasa kwenye sekta ya elimu bila kuyumba, kutetereka wala kuogopa.

Kadhalika, Waziri Mkenda amempongeza Mbunge wa Jimbo la Chalinze ambaye ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Ridhiwani Kikwete kwa juhudi zake za kuliendeleza Jimbo lake katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo na elimu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maemdleeo ya Makazi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Chalinze Mhe Ridhiwani Kikwete amempongeza Waziri Mkenda kwa uthubutu wake wa kuamua kufanya mabadiliko katika sekta ya elimu ambao utakuwa chachu kubwa katika kuikuza na kuiendeleza sekta ya elimu nchini.

“Uthubutu huo ndio ambao una kielelezo cha kutosha kuelekea kwenye maendeleo ambayo kila mtanzania anayataka, Rais yetu Mhe mama Samia Suluhu Hassan alipoamua kumchagua Prof Mkenda kuwa waziri wa elimu, mimi binafsi nilifurahi sana” Amekaririwa Mhe Kikwete

Naibu Waziri Kikwete amesema kuwa kilichomfurahisha kwa kuteuliwa Prof Mkenda kuwa Waziri ni rekodi yake nzuri aliyoiacha Chuo kikuu huku akimtaja kuwa kiongozi wa mfano kwa wanasiasa wanaochipukia.

“Wapo watu wachache ambao wanaweza wakabeza mambo unayoyafanya kwenye nchi hii lakini nia yako itashinda hayo ambayo watu wengine wanafikiri juu yako. Siku zote kwenye maendeleo weka mipango kwanza, tafakari jinsi ya kufanya na tekeleza mipango hiyo na wewe Prof Mmenda umekuwa ukifanya hivyo” Amesisitiza

Mhe Ridhiwani amesema kuwa ataendelea kuunga mkono juhudi za Waziri Mkenda katika utekeleza mabadiliko ya elimu anayoyafanya ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta ya elimu nchini.

“Mimi naamini tukikusaidia wewe maana yake tumemsaidia Mheshimiwa Rais, na amekuteua wewe kwa sababu anajua kabisa kuwa ili ufanikiwe lazima uwe na watu nyuma yako na sisi tupo nyuma yako” Amesisitiza Ridhiwani

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!