Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Mohamed Bashe (Mb) na Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji leo tarehe 16 Julai, 2022 wametembelea viwanda vitatu vinavyoongeza thamani mazao ya kilimo, vyote vya Morogoro mjini.
Viwanda walivyotembelea ni Mahashree Agro – Processing Tanzania Ltd (Kiwanda cha kuongeza thamani mazao karanga, karafuu, mbaazi, dengu, choroko na ufuta); Alliance One na Mkwawa Leaf Tobacco – zamani TLTC) vyote vya kusindika tumbaku.
Wakiwa katika viwanda hivyo; Mawaziri wote wamesikiliza mafaniko na changamoto wanazokutana nazo Wawekezaji na kuwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na rahisi ili kulinda uwekezaji wao.
Aidha, Waziri Bashe amewataka Wamiliki wa viwanda hivyo kuhakikisha wanalinda maslahi ya Wakulima ili kuongeza ustawi wa katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.
Waziri Bashe ametoa wito kwa Wakulima wa tumbaku kujiandaa kulima kwa wingi zao hilo kwa kuwa soko la tumbaku la zaidi ya tani 140,000 limefungua kutokana na kufunguliwa kwa kiwand cha Mkwawa Tobacco Ltd na kiwanda cha Alliance One ambavyo kila kiwanda kina uwezo wa kusindika tani 70,000.
“Wakulima wa tumbaku limeni kwa kuwa soko lipo, nimeshawaagiza TORITA (Taasisi ya Utafiti wa Tumbaku) kazi ya kuzalisha mbegu bora za tumbaku, mbegu zitakapokuwa tayali, tutawapa Wakulima ili waongeze tija na uzalishaji”. Amesisitiza Waziri Bashe.
Waziri Bashe amewataka Wakulima wa mazao ya mikunde na viungo pamoja na ufuta kuendelea kulima kwa wingi kwa kuwa soko la uhakika lipo kupitia kiwanda cha Mahashree Agro – Processing Tanzania Ltd ambacho kina uwezo wa kusindika tani 200 za mazao hayo kwa siku.
Kiwanda cha Mahashree Agro – Processing Tanzania Ltd kina mashine za kisasa za kusindika mazao ya karanga, karafuu, mbaazi, dengu, choroko na ufuta.
Kwa upande wake Waziri wa Uwekezaji Viwanda Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali ya Awamu ya Sita ipo kwa ajili ya kujenga mazingira mazuri kwa wenye viwanda na kuongeza kuwa msingi wa ziara yake na Waziri wa Kilimo ni kusikiliza kero za Wawekezaji na kuzitatua.
“Niwahakikishie Wawekezaji kuwa tupo hapa ajili ya kujenga Tanzania ya viwanda kivitendo; Tunasikiliza kero za Wawekezaji na tumejipanga kuzitatua. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshafanya kazi kubwa ya kuvutia Wawekezaji, kazi yetu ni kuhakikisha tunajenga mazingira mazuri kwa Wawekezaji”. Amekaririwa Waziri Dkt. Ashatu.