Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Adolf Mkenda amezindua Bodi ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) leo tarehe 11 Novemba, 2022, jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo, Mhe. Prof. Mkenda ameipongeza Bodi iliyomaliza muda wake kwa kusimamia vizuri utendaji wa Baraza ikiwemo uendeshaji wa mitihani huku akiitaka Bodi hiyo kuendeleza mazuri yaliyofanyika na watangulizi.
“Nataka kusema Bodi iliyomaliza muda wake imetekeleza kwa mafanikio anzieni walipoishia na boresheni zaidi.,” amesema Prof. Mkenda.
Aidha, Prof. Mkenda, amesema bado kuna changamoto kwenye kusimamia mitihani hususani inapopelekwa kwenye vituo vya kufanyia mitihani na kuitaka bodi mpya kuhakikisha inasimamia ili kuondoa changamoto.
Waziri amewataka Wajumbe wa Bodi kuziangalia Kamati za Mitihani kwa ngazi ya Wilaya na Mikoa kuona kama kuna haja ya kuziboresha ama la.
“Kamati za Mitihani zinafanya kazi kubwa sana kusimamia mitihani mingi, lakini kuna haja ya kuona kama Kamati hizo zinajitosheleza au kuna haja ya kuingiza watu wengine ili kuongeza ufanisi katika kusimamia mitihani,” amesisitiza Prof. Mkenda.
Pia Prof. Mkenda amelipongeza Baraza la Mitihani kwa kuanzisha mfumo wa usahihihshaji mitihani kidigitali ‘E-Marking’ na kuwataka watalaam kuendelea kuuboresha ili kuongeza usalama wake.
Prof. Mkenda amempongeza Prof. William Anangisye kwa kuteuliwa tena na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Mitihani.
Kwa upande wake, Prof. Anangisye ameshukuru kwa kuteuliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Baraza na kuhaidi Bodi yake kushirikiana na Menejimenti na wadau wa Elimu kuhakikisha Baraza linasonga mbele.