Home Kitaifa WAZIRI MKUU AKABIDHI MIKOPO KWA VIKUNDI VYA WAJASIRIAMALI RUANGWA

WAZIRI MKUU AKABIDHI MIKOPO KWA VIKUNDI VYA WAJASIRIAMALI RUANGWA

Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo Julai 08, 2022 amekabidhi mikopo yenye jumla ya shilingi, 256,158,000 iliyotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa vikundi 27 vyenye wanufaika 196. Kati ya vikundi hivyo vya wanawake ni 14 ambavyo vimepewa mkopo wa shilingi 36,126,000. Vikundi vinane vya vijana vilipata mkopo wa shilingi 213,532,000 na vikundi vitato vya watu wenye ulemavu vilipata mkopo wa shilingi 6,500,000.

Akizungumza na wakazi wa kata ya Mandawa wilayani Ruangwa baada ya kukabidhi mikopo hiyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa matumizi mazuri ya asilimia 10 ya makusanyo yao ya ndani ambayo yanatakiwa yatolewe mkopo kwa vikundi vya vijana (asilimia nne), wanawake (asilimia nne) na wenye ulemavu (asilimia mbili).

Waziri Mkuu amesema uamuzi wa halmashauri hiyo kutoa mkopo huo utaviwezesha vikundi hivyo kuongeza mitaji na uwezo wa kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali. “Vikundi vimewezeshwa kwa kuongezewa mitaji itakayoviwezesha kuzalisha kwa tija na kuweza kurejesha mikopo kwa wakati ili waweze kukopeshwa wengine.”

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Frank Chonya amesema kati ya fedha hizo shilingi 214,658,000 zimetolewa kwa vikundi sita vya kimkakati ambapo kati yake vikundi vitatu vya vijana vinavyojishughulisha na usafirishaji wa abiria wa pikipiki vyenye wanufaika 20 vimepewa mkopo wa shilingi 57,132,000 zilizotumika kununua pikipiki 20.

Kikundi kimoja cha vijana wa Kata ya Mandawa ambacho kina vijana 20 wanaojishughulisha na ufyatuaji wa tofali kimepewa mkopo wa shilingi 145,400,000 na kimenunua lori la tani nane litakalotumika kubebea mchanga na matofali. Pia kimenunua mashine ya kisasa ya kufyatulia matofali yenye thamani ya shilingi 25,000,000 pia kimekopeshwa shilingi 10,000,000  kama mtaji.”

Amesema ili kurahisishia soko, Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa itakuwa inanunua matofali kutoka kwa vijana hao kwa ajili ya ujenzi miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali katika wilaya hiyo. Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya na elimu.

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa vikundi vingine viwili vinavyojishughukisha na ufugaji kuku vyenye wanufaika 17 vilipewa mkopo wa shilingi 12,126,000 uliowawezesha kununua kuku 800 pamoja na vyakula vya kuku na dawa.

Pamoja na kutoa mikopo kwa vikundi vya kimkakati halmashauri imeendelea kutoa mikopo kwa vikundi vidogovidogo.”
Amesema mikopo yenye thamani ya shilingi 41,500,000 imetolewa kwa vikundi 20 vyenye wanufaika 133 ambapo kati yake vikundi vya vijana vine vyewe wanufaika 22, wanawake vikundi 12 vyenye wanufaika 95 na vikundi viwili vya watu wenye ulemavu vyenye wanufaika 16.

Kupitia utoaji huu wa mikopo jumla ya ajira 452 zimepatikana katika mwaka wa fedha 2020/2021 na mwaka 2021/2022 hivyo kupunguza uzululaji, uhalifu na utegemezi kwa vijana.”

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mandawa Issa Lipei ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!