Home Kitaifa WAZIRI MKENDA AGEUKA MBOGO UCHAGUZI WA SKAUTI

WAZIRI MKENDA AGEUKA MBOGO UCHAGUZI WA SKAUTI

Mlezi wa SKAUTI ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ana matumaini na matarajio makubwa kwa Chama cha SKAUTI nchini kuwa eneo muhimu la malezi na ukakamavu kwa vijana.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 2 Julai 2022 katika ukumbi wa Chuo cha Mipango Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa uchaguzi wa Chama cha SKAUTI Tanzania.

Waziri Mkenda ametoa salamu za Rais Samia mbele ya wajumbe hao na kuwakumbusha kuwa uchaguzi huo unapaswa kuwa kielelezo cha uchaguzi wa viongozi bora wenye weledi, nidhamu na mshikamano miongoni mwao.

Amesema kuwa Rais Samia ameahidi kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Kimataifa cha SKAUTI nchini na kuendeleza malezi bora kwa vijana kama mlezi wao.

Waziri Mkenda amekemea makandokando yaliyopo kwenye chama hicho na kusisitiza kuwa “Tuhakikishe leo ni mara ya mwisho kabisa kwa SKAUTI Tanzania kupata mafua na tufungue ukurasa mpya wa kusimamia kazi kubwa ambazo zimefanywa na viongozi waliomaliza muda wao”

“Hatuwezi kuwa na SKAUTI ambayo kwa hiyari yake na katiba yake imemuweka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mlezi halafu sisi tufanye mchezo mchezo, tunataka apende, afurahie kuwa mlezi wetu asione kama SKAUTI ni kero ambayo anatamani kuitua ili akabidhi mahali pengine” Amekaririwa Waziri Mkenda

Waziri Mkenda amesema kuwa haiwezekani kuwa na SKAUTI yenye majina ya heshima kama Rais mstaafu wa Tanzania Mhe Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania Mhe Dkt Salim Mohamed Salim, Shekh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakar Zubeir Bin Ally, Kiongozi wa kanisa katoliki Tanzania Polycarp Kadinari Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki Mbeya Mhashamu Baba Askofu Gervas Nyaisonga halafu kufanyike mzaha mzaha, hivyo atasimamia maadili ipasavyo.

Waziri Mkenda amesema kuwa nidhamu na uadilifu wa SKAUTI unapaswa kuonekana jinsi kazi inavyofanywa ”SKAUTI ina afya lakini ina mafua sio mazuri na leo ni mara ya mwisho SKAUTI kuwa na Sokomoko kama viatu vya mpira kwani limesababisha sisi kuchukua hatua ambazo sio za kawaida ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya mpito” Amesema Prof Mkenda

Katika hatua nyingine Waziri Mkenda amesema kuwa kumekuwa na mapendekezo mengi kutoka kwa wajumbe wa SKAUTI wakiomba Rais mstaafu wa Tanzania Mhe Jakaya Mrisho Kikwete kujiunga na Bodi ya wadhamini wa SKAUTI.

Amesema kuwa ni heshima kubwa kwa viongozi wakubwa kama hao kuwekwa kwenye nafasi hizo muhimu kwa maslahi ya Taifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!